Sifuna amtaka waziri Ababu Namwamba kushughulikia matatizo katika wizara yake

Waziri Ababu alisema yeye ndiye waziri ambaye amefanya ziara chache sana nje ya nchi.

Muhtasari

• Sifuna alisema mara nyingi wakati Timu ya Kenya inaposafiri kwa mashindano nje ya nchi, huwa wanakosa mahitaji mengi muhimu na kuongeza kuwa viongozi wengi wa serikali huwa hawapo karibu na wachezaji kuwaunga mkono.

b6251efb2cdb00bc
b6251efb2cdb00bc

Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna amemtaka Waziri wa Michezo Ababu Namwamba kushughulikia matatizo mengi yanayoathiri Wizara hiyo ambayo bado hayajatatuliwa.

Akiongea Ijumaa wakati wa mahojiano kwenye Spice FM, Sifuna alisema amejaribu kuibua masuala mbalimbali katika seneti kuhusu changamoto katika sekta ya michezo lakini hadi sasa hakuna kilichofanyika.

"Kuhusu suala la michezo, nadhani kila mtu anakubali kwamba kuna tatizo. Ndugu yangu Ababu Namwamba hana budi kujizatiti zaidi," alisema.

Sifuna alisema mara nyingi wakati Timu ya Kenya inaposafiri kwa mashindano nje ya nchi, huwa wanakosa mahitaji mengi muhimu na kuongeza kuwa viongozi wengi wa serikali huwa hawapo karibu na wachezaji kuwaunga mkono.

"Katika maisha yangu mengine, nilikuwa msimamizi wa timu ya raga ya wanawake. Walipokuwa wakienda Madagaska, nilikuwa afisa wa ngazi ya juu wa serikali ambaye alitembelea timu kabla ya kuondoka," Sifuna alisema.

Alisema wanariadha hata hukosa taarifa muhimu kama vile maelezo ya safari zao. Alishikilia kuwa nchi haijatambua kikamilifu uwezo wa michezo kwani uchumi hauwapi vijana njia mbadala.

“Angalia michezo ya Shule za Sekondari za Kenya iliyofanyika Kakamega, wengi walijitokeza kutazama michezo hiyo na hiyo inaonyesha nia na vipaji vipo...Mara moja mashirika makubwa yalipogundua kuwa kulikuwa na umati mkubwa hapo ndipo yalipoanza kuonekana,"Sifuna alieleza.

Namwamba mnamo Agosti 23 alikanusha madai kwamba amekuwa akizunguka ulimwengu huku akitelekeza wanamichezo.

Akijibu maswali ya wabunge kuhusu madai ya kuwatelekeza wanariadha, Waziri huyo alisema yeye ndiye waziri ambaye amefanya ziara chache sana nje ya nchi.

"Si kweli kwamba ninazuru dunia. Naweza kuthibitisha kwa bunge hili kwamba kutokana na hatua za matumizi zilizochukuliwa ndani ya wizara, sijawahi kupata nafasi ya kuambatana na timu zetu zinazosafiri nje ya nchi," alisema