ODM yamtoza Passaris faini ya Sh250k kwa kuunga mkono Mswada wa Fedha

"Pamoja na hayo, Passaris atozwe faini ya Sh250,000 ambayo inapaswa kulipwa ndani ya siku 60."

Muhtasari
  • Chama hicho kilisema NEC iliitishwa baada ya mfululizo wa vikao vilivyofanywa na vyombo vingine vya chama vikiwemo Kamati Kuu ya chama
  • Chama hicho kilisema pia kitawaadhibu wabunge ambao hawakuwapo wakati wa zoezi la upigaji kura.
Image: EZEKIEL AMING'A

Chama cha ODM kimemtoza faini Mwakilishi wa Wanawake wa Nairobi Esther Passaris kwa kwenda kinyume na msimamo wa chama na kupigia kura Mswada wa Fedha wa 2023, ambao sasa ni Sheria.

Katika taarifa yake Jumatano, chama hicho kilisema Passaris atalazimika kulipa Sh250,000 kama faini kwa kukaidi chama kando na kuomba msamaha kwa maandishi ndani ya siku saba.

Chama hicho kilisema azimio hilo lilifikiwa wakati wa Kamati Kuu ya Kitaifa ya chama hicho iliyofanyika Jumatano chini ya uongozi wa kiongozi wa Chama Raila Odinga.

 

"Kwamba Esther Passaris, Mbunge wa Kike katika Kaunti ya Nairobi akaripiwe kwa kukaidi moja kwa moja msimamo wa chama kuhusu Mswada wa Sheria ya Fedha wa 2023 na kwamba anapaswa kuomba radhi kwa maandishi ndani ya siku saba," chama hicho kilisema.

"Pamoja na hayo, Passaris atozwe faini ya Sh250,000 ambayo inapaswa kulipwa ndani ya siku 60."

Chama hicho kilisema NEC iliitishwa baada ya mfululizo wa vikao vilivyofanywa na vyombo vingine vya chama vikiwemo Kamati Kuu ya chama, Kamati ya Nidhamu na Bodi ya Taifa ya Uchaguzi.

Mkutano huo uliongozwa na Mwenyekiti wa Kitaifa John Mbadi.

Passaris alikuwa miongoni mwa wanachama 28 wa Orange Democratic Movement ambao walikaidi chama na kuupigia kura Mswada huo mnamo Juni 14.

Chama hicho kilisema pia kitawaadhibu wabunge ambao hawakuwapo wakati wa zoezi la upigaji kura.

Wakati wa upigaji kura, Wabunge 176 waliunga mkono Mswada wa Fedha katika Kusomwa Mara ya Pili na 81 pekee waliupinga.

Siku iliyofuata mnamo Juni 15, katibu mkuu wa chama hicho Edwin Sifuna alisema wanachama wanne wa ODM waliunga mkono Mswada huo huku wengine 24 hawakuhudhuria wakati wa kupiga kura.

"Kwa hivyo Chama kimeanzisha mashauri ya kinidhamu dhidi ya wanachama," Sifuna alisema.

Akizungumza nje ya Bunge baada ya Kusomwa kwa Bajeti ya Mwaka wa Fedha wa 2023-2024, Passaris alisema bado ni mwanachama mwenye bidii wa ODM licha ya msimamo wake kuhusu Mswada huo.