Afisa mmoja wa polisi alifariki Jumatano kwa kujitoa uhai baada ya kujipiga risasi kichwani katika makao makuu ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) jijini Nairobi.
Wenzake walisema alijifungia ndani ya gari lake na kujipiga risasi kichwani kwa bastola yake kwenye eneo la maegesho. Alikufa papo hapo.
Haijabainika mara moja sababu ya afisa huyo amabye ni dereva wa polisi alichukua hatua hiyo kali. Wenzake waligutushwa na mlio wa risasi kutoka sehemu ya kuegesha magari kwenye sehemu ya shughuli na waliposongea walimkuta tayari amekufa.
Risasi ilimpasua kichwa. Mwili wake ulihamishwa hadi katika chumba cha kuhifadhia maiti ukisubiri kufanyiwa uchunguzi. Maafisa wakuu walikuwa ofisini wakati wa kisa hicho. Kulikuwa na hofu kuhusu mkasa huo.
Hili ni tukio la hivi punde zaidi kutokea katika huduma ya polisi. Wiki iliyopita, afisa mkuu alifariki kwa kujitoa uhai nyumbani kwake eneo la Utawala, Nairobi.
Superintendent Ezra Ouma alijipiga risasi nyumbani kwake alasiri ya Alhamisi Oktoba, 5 muda mfupi baada ya kumpigia simu rafiki yake ambaye pia ni afisa wa polisi na kumwambia angekufa kwa kujiua.
Ouma alikuwa msimamizi wa ofisi ya operesheni maalum (SOB) katika kituo cha polisi cha Kayole. Alikuwa anastaafu katika kipindi cha miaka miwili, wenzake walisema. Polisi walifika eneo la tukio walisema Ouma pia alimpiga risasi jirani yake kwenye mguu wake wa kushoto baada ya kujaribu kumzuia kutojiua.
Makumi ya maafisa wa polisi wamekufa kutokana na kujitoa uhai katika hali inayohusishwa na msongo wa mawazo kazini. Kama sehemu ya juhudi za kukabiliana na hali hiyo, mamlaka ya polisi imezindua huduma za ushauri nasaha na Tume ya Kitaifa ya Huduma ya Polisi imeanzisha kitengo na kukipa wafanyikazi kushughulikia hali yao ngumu.
Kitengo cha ushauri nasaha, miongoni mwa mambo mengine, kitatathmini, kubuni na kuongoza programu ya kufikia watu ambayo husaidia kuzuia afya ya akili na matumizi mabaya ya dawa za kulevya.
Angalau visa vitatu vya kujitia kitanzi vinavyohusisha maafisa wa polisi hurekodiwa kila mwezi. Maafisa wanasema polisi kwa ujumla huwa wanakabiliana na matatizo yote ya jamii. Wanatarajiwa kudumisha sheria na utulivu katika hali ngumu sana, kando na kuweka maisha yao hatarini.
Kwa miaka mingi, ongezeko la vifo katika huduma hiyo limehusishwa na msongo wa mawazo na mazingira duni ya kufanyia kazi.