Kamati ya Seneti inayochunguza vifo vya Shakahola imetembelea Kanisa la New life Prayer Center inayoogozwa na Mchungaji Ezekiel Odero.
Kamati hii ya muda yenye maseneta 11 inayoongozwa na Seneta wa Tana River, Danson Mungatana ilitua kwenye uwanja wa ndege wa Mombasa mwendo wa saa mbili unusu asubuhi na wakaelekea moja kwa moja hadi Mavueni, ambako ni makao makuu ya kanisa hilo.
Ezekiel Odero siku chache zilizopita alifanyiwa mahojiano ya moja kwa moja na kamati ya seneti ili kujibu mahusiano yake na mchungaji mwenye utata Paul Mackenzie wa Kanisa la Good News International.
Mchungaji huyu aliwaomba maseneta kuzuru kanisa lake lililoko Mavueni kaunti ya Kilifi ili kufanya uchunguzi wao jinsi shughuli za maombi zinafanyika katika kanisa hilo
Wakati wa mahojiano ya moja kwa moja katika seneti , Ezekiel alikiri kutokuwa na uhusiano wowote na mchungaji mwenye utata Paul MacKenzie ambaye alidaiwa kusababisha vifo zaidi ya mia nne kupitia kile kilichodaiwa kuwashirikisha wafuasi wake katika mfungo wa imani .
Ezekiel alielezea seneti kuwa kanisa lake lina zaidi ya washirika 45,000. Mchungaji huyo alitakiwa kueleza jinsi alivyomiliki zaidi ya Akaunti tano za benki .
"Washirika wangu wanapotoa sadaka sisi kama kanisa la Newlife tunafanya kikao na wakuu wa kanisa ili tuweze kujadiliana jinsi ambavyo tutasaidia wakazi wa Kilifi kupitia ajira mfano tumefungua Hoteli ambayo ni ajira kwa wengi," alisema mchungaji huyo.