Waziri wa Nishati Davis Chirchir amesema kuwa huenda bei ya mafuta ya super petroli ikaongezeka hadi kufikia shillingi mia tatu ikiwa bei ya kimataifa itaongezeka.
"Bei za kimataifa za mafuta zinaweza kupanda hadi dola 150,Hii inamaanisha kuwa bei zetu za petroli zinaweza kupanda hadi Sh300 kwa lita kwenye Bomba,Tunatumai haitafika huko," alisema.
Waziri huyo alisema hayo alipokuwa akizungumza mbele ya kamati ya Mazungumzo ya Kitaifa Bomas of Kenya Jumatatu.
Katikati mwa mwezi Oktoba, Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Petroli nchini Kenya ilitangaza bei mpya ya mafuta hadi rekodi ya juu katika historia ya nchi, lita moja ya petroli sasa ikiuzwa kwa Sh217.
Kupanda kwa bei ya mafuta kwa upande wake kutasababisha kupanda kwa bei za bidhaa zingine, hatua iliyoibua kejeli mbalimbali kutoka kwa wananchi waliolalamikia ughali wa maisha.
Kenya na Afrika Kusini zimekuwa zikikabiliwa na ongezeko la gharama ambalo limechangiwa na tatizo la ongezeko la mafuta duniani.
Kulingana na Mtazamo wa hivi karibuni wa Masoko ya Bidhaa mzozo wa Israel na Gaza umechangia pakubwa katika bei ya bidhaa kupanda kutokana na kukatika kwa mzunguko wa kimataifa wa usambazaji bidhaa.