Shakahola: Pasta Mackenzie kusalia kizuizini kwa mwezi mmoja zaidi

DPP Yamina pia alipinga kuachiliwa kwa washukiwa sita kati ya 29 wa Shakahola kama ilivyopendekezwa katika ripoti za uchunguzi wa kijamii

Muhtasari

• Mkurugenzi Msaidizi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Jami Yamina aliorodhesha sababu kadhaa za msingi za washukiwa hao  kuzuiliwa hadi  pale uchunguzi utakapo malizika.

• Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, sheria za ugaidi zinaruhusu hadi siku 360 za kizuizini halali kusubiri kukamilika kwa uchunguzi

Mchungaji Paul Mackenzie
Mchungaji Paul Mackenzie Mchungaji Paul Mackenzie

 Paul Mackenzie, mshukiwa mkuu wa mauaji ya halaiki katika shamba la Shakahola, na watuhumiwa wenzake 28 watasalia kwenye rumande hadi Desemba 22, 2023 mahakama itakapotoa uamuzi kuhusu ombi la serikali la kutaka wazuiliwe kwa siku 180 zaidi wakisubiri kufunguliwa mashtaka.

Katika ombi hilo, Mkurugenzi Msaidizi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Jami Yamina aliorodhesha sababu kadhaa za msingi za washukiwa hao  kuzuiliwa hadi  pale uchunguzi utakapo malizika.

Aidha, alisema kwa kuwa washtakiwa awali walitishia kujitia kitanzi, kuzuiliwa  itakuwa njia  ya kipekee itakayo wezesha uchunguzi kufanyika na kukamilika ili mashtaka kufunguliwa dhidi yao.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, sheria za ugaidi zinaruhusu hadi siku 360 za kizuizini halali kusubiri kukamilika kwa uchunguzi na bunge hilo. Kwa hekima yake, iliongeza siku kutoka siku 90 hadi siku 360 ili kushughulikia kesi ngumu.

Jami pia alipinga kuachiliwa kwa washukiwa sita kati ya 29 wa Shakahola kama ilivyopendekezwa katika ripoti za uchunguzi wa kijamii uliofanywa na idara ya Probation and Aftercare Services.

Alimweleza Hakimu Mkuu Mwandamizi Yusuf Shikanda kuwa watuhumiwa hao wanatakiwa kufanyiwa uchunguzi kabla ya kurejeshwa kwenye jamii na wanafamilia wao hawajatoa maelezo ya kudhibitisha kuwa hawatajidhuru.

Zaidi ya miili 420 ya ibada ya siku ya maangamizi ya Mackenzie, ambapo wafuasi walihimizwa kujiua kwa njaa ili ‘kumlaki Yesu’ imefukuliwa kufikia sasa..