Kanisa la Mackenzie ni kundi la kihalifu, Kindiki atangaza

Dhehebu hilo linashukiwa kuhusika na vifo vya zaidi ya watu 400 vilivyotokea kati ya Januari 2021 na Septemba 2023.

Muhtasari

• Mchungaji Mackenize na washtakiwa wengine zaidi ya tisini wanakabiliwa na mashtaka 238 yakiwemo ugaidi.

Image: CHARLES MGHENYI

Waziri wa Mambo ya Ndani (CS) Kithure Kindiki ametangaza dhehebu la Good News International Ministries lake mhubiri Paul Mackenzie kuwa kikundi cha uhalifu. 

Katika taarifa yake aliyoitoa Jumatano, Kindiki alisema hatua hiyo ni kwa mujibu wa Kifungu cha 22(1) cha Sheria ya Kuzuia Uhalifu wa Kupangwa. Kifungu kilichotajwa kinaelekeza kwamba “Endapo Waziri ana sababu za msingi za kuamini kuwa kikundi fulani kinajihusisha na uhalifu wa kupangwa anaweza, kwa ushauri wa Kamishna wa Polisi, kwa notisi, kutangaza kuwa kundi fulani ni la kihalifu uliopangwa.   

Dhehebu hilo lenye makao yake katika eneo la Shakahola, Kaunti ya Kilifi, ndiyo ngome ya dhehebu linaloshukiwa kuwa limehusika na vifo vya zaidi ya watu 400 vilivyotokea kati ya Januari 2021 na Septemba 2023. 

Mchungaji Mackenize na washtakiwa wengine zaidi ya tisini wanakabiliwa na mashtaka 238 yakiwemo ugaidi na itikadi kali. Wamekana mashtaka yote. 

Mackenzie na washtakiwa wenzake ambao wamekaa rumande kwa miezi kadhaa, wataendelea kusalia rumande kufuatia ombi la upande wa mashtaka la kutaka kuendelea kuwazuilia hadi kukamilika kwa upelelezi.