Khalwale asema siasa imeingizwa kwa kifo cha mfanyikazi wake

Khalwale aliomba idara husika za serikali kufanya uchunguzi wa kina kubaini kilichomuua Moi.

Muhtasari

• “Tutamalizana na tutakabiliana wenyewe kisiasa. Nimewakabili hapo nyuma nikawashinda na tena mara hii nitawaibisha”, Khalwale alimalizia.

Dr Boni Khalwale Seneta Kaunti ya Kakamega Picha: HISANI
Dr Boni Khalwale Seneta Kaunti ya Kakamega Picha: HISANI
Image: MAKTABA

Seneta wa Kakamega Bonny Khalwale sasa anadai kuwa wapinzani wake wameingiza siasa katika kifo cha mfanyikazi wake Kizito Moi.

Akizungumza nyumbani kwa marehemu Khalwale aliomba idara husika za serikali kufanya uchunguzi wa kina kubaini kilichomuua Moi.

“Hii si matanga ya Moi, hii ni siasa tupu. Na nataka kushukuru serikali kwa kuona kwamba hii si matanga ni Siasa. Kama haingekuwa siasa Nairobi haingekuwa inakuja hapa. Wako na DCI hapa Malinya, alikuja akafanya kazi yake akamaliza”, Khalwale alisema.

Seneta huyo alisema kwamba mara ya kwanza afisa wa DCI kutoka Malinya alifika kwa boma lake akafanya uchunguzi akamaliza na kuandika ripoti yake. Aliongeza kuwa walienda hadi mochari ambapo mwanapatholojia wa Kakamega alifanya uchunguzi na kuthibitisha kilichomuua mfanyikazi huyo.

“Laskini kwa sababu siasa illingia ilibidi DCI wa Malinya arudi mara ya pili, amemaliza. Leo imerudi DCI wa Region chief inspector Daniel  amekuwa hapa amefanya a thourough process amemaliza. Sasa vile unaona inaenda Nairobi ni siasa”, Khalwale alieleza.

Baada ya matanga Khalwale aliahidi kuwakabili wale wote waliongiza siasa kwa mkasa huu.

“Tutamalizana na tutakabiliana wenyewe kisiasa. Nimewakabili hapo nyuma nikawashinda na tena mara hii nitawaibisha”, Khalwale alimalizia.

Khalwale alijawa na hisia kali wakati akitangaza habari za kusikitisha kuhusu jinsi fahali wake wa kupigana alivyomuua mlezi wake Jumamosi iliyopita.

Marehemu, Kizito Moi kulingana na ripoti iliyowasilishwa na Seneta katika kituo cha polisi cha Malinya alikuwa na umri wa miaka 46.

Kulingana na Khalwale, mwili huo ulipatikana kwenye zizi la ng'ombe na mfanyakazi mwingine alipokuwa akizunguka kutekeleza majukumu yake.

Akizungumza baada ya kisa hicho, mwanasiasa huyo alisema fahali huyo huenda alimvamia mfanyikazi huyo usiku alipomrejesha kwenye zizi la ng’ombe.