Seneta Khalwale azidiwa na hisia baada ya fahali wake mpiganaji kumuua mfanyakazi wake

Khalwale alieleza kuwa fahali anayemuua anayemchunga lazima achinjwe kisha nyama igawanywe miongoni mwa wanakijiji.

Muhtasari

•Khalwale alijawa na hisia kali wakati akitangaza habari za kusikitisha kuhusu jinsi fahali wake wa kivita alivyomuua mlezi wake siku ya Jumamosi.

•Mwili wa Moi ulipatikana kwenye zizi la ng'ombe na mfanyakazi mwingine alipokuwa akizunguka kutekeleza majukumu yake.

akiwahutubia wanahabari baada ya fahali wake kumuua mfanyikazi wake siku ya Jumamosi, Januari 27, 2024.
Boni Khalwale akiwahutubia wanahabari baada ya fahali wake kumuua mfanyikazi wake siku ya Jumamosi, Januari 27, 2024.
Image: HISANI

Seneta wa Kakamega Boni Khalwale alijawa na hisia kali wakati akitangaza habari za kusikitisha kuhusu jinsi fahali wake wa kivita alivyomuua mlezi wake siku ya Jumamosi.

Mwanasiasa huyo wa UDA aliomboleza marehemu Kizito Moi Amukune kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii huku akifichua kuwa mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 46 alikuwa amewachunga mafahali wake kwa takriban miongo miwili

“Fahali wangu bingwa, Inasio, amemvamia na kumuua papo hapo Kizito Moi Amukune. Moi amekuwa mlezi wa ng'ombe wangu wa kivita kwa zaidi ya miaka 20. Kwa kuzingatia tamaduni zetu, leo nimemuua fahali Inasio,” Khalwale alishiriki kwenye X.

Seneta aliambatanisha taarifa yake na video zake na wanakijiji wakifanya matambiko yanayofanywa na jamii baada ya tukio la aina hiyo kutokea.

Kulingana na ripoti ya polisi iliyofikia Radio Jambo, kisa hicho kilitokea katika makazi yake katika kijiji cha Shikhuyu, Kitongoji cha Shitoli, kaunti ya Kakamega.

Marehemu, Kizito Moi kulingana na ripoti iliyowasilishwa na Seneta katika kituo cha polisi cha Malaika alikuwa na umri wa miaka 46.

"Maafisa wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Malaika na maafisa wa DCI walitembelea eneo la tukio na kubaini kuwa kweli kulikuwa na mwili wa Kizito Moi mwenye umri wa miaka 46 ambaye alikuwa mlezi wa ng'ombe dume anayeitwa Inasio mwenye umri wa miaka 5 na uzani wa takriban kilo 520," ripoti ya polisi inasoma.

"Mwili ulikuwa na majeraha mengi yanayoshukiwa kusababishwa na fahali huyo. Eneo la tukio lilifanyiwa kazi na mwili huo kuhamishiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Kakamega ukisubiri kufanyiwa uchunguzi."

Kulingana na Khalwale, mwili huo ulipatikana kwenye zizi la ng'ombe na mfanyakazi mwingine alipokuwa akizunguka kutekeleza majukumu yake.

Akizungumza baada ya kisa hicho, mwanasiasa huyo alisema fahali huyo huenda alimvamia mfanyikazi huyo Jumamosi usiku alipomrejesha kwenye zizi la ng’ombe.

Aliongeza kuwa mwili wake ulipatikana Jumapili asubuhi.

Kulingana na mila za Waluhya, Khalwale alieleza kuwa fahali anayemuua mtu anayemchunga lazima achinjwe kisha nyama igawanywe miongoni mwa wanakijiji.

"Kwa kuzingatia utamaduni wetu, kwa kumuua mlezi wake, ng'ombe bingwa, Inasio anafikia mwisho wake kwa nguvu ya mkuki wangu," Seneta alisema.

Khalwale alionyesha ng'ombe huyo akisindikizwa na wanakijiji hadi mahali ambapo alikutana na kifo chake kwa njia ya mkuki. Kisha nyama iligawanywa kati ya wanakiji.