Mwanamke afariki baada ya kuchomwa kisu na mumewe katika ugomvi wa ndoa

Ugomvi ulizuka na mwanamume huyo akachukua kisu na kumchoma Chepkemoi upande wa kushoto wa shingo.

Muhtasari

•Marehemu alikuwa ameondoka nyumbani kwa mshukiwa kwa familia yake baada ya kutofautiana kinyumbani.

•Polisi walitembelea eneo la tukio na kupata mshukiwa amekamatwa na chifu wa eneo hilo na wenyeji.

Crime scene
Crime scene
Image: HISANI

Polisi wanamshikilia mwanamume mwenye umri wa miaka 27 kwa madai ya kumdunga kisu mkewe nyumbani kwa wazazi wake katika eneo la Kipsolu, Kaunti ya Kericho kuhusu mzozo wa ndoa.

Tukio hilo lilitokea Ijumaa, Januari 26.

Mshukiwa alikuwa amesafiri kutoka Borborwet hadi nyumbani kwa mkewe ili kutatua masuala yao ya nyumbani.

Mwanamke aliyefariki ambaye alitambulika kama Lonah Chepkemoi, 27 alikuwa ameondoka nyumbani kwa mshukiwa kwa familia yake baada ya kutofautiana kinyumbani.

Hii ilimlazimu mshukiwa kumfuata marehemu nyumbani kwa mzazi wake ili kutatua masuala yao ya nyumbani.

Katika harakati hizo, ugomvi ulizuka na mwanamume huyo akachukua kisu na kumchoma Chepkemoi upande wa kushoto wa shingo.

Hii iliwalazimu waliokuwepo kukimbilia usalama wao kabla ya kurudi.

Alikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Kericho ambako alitangazwa kuwa amefariki alipofika, polisi walisema.

 

Walifanikiwa kupata kisu kimoja cha jikoni kilichokuwa na damu kinachoshukiwa kutumiwa na mshukiwa wa mauaji hayo.

Maafisa hao walifyatua risasi mbili hewani kutawanya umati na kurejesha utulivu walipokuwa wakitaka kumuangamiza..

Mwili wa mwanamke huyo ulihifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti ukisubiri kufanyiwa uchunguzi.

Katika kisa kingine, polisi katika Kaunti ya Kiambu wanachunguza kisa ambapo mfungwa mwenye umri wa miaka 24 anaripotiwa kufariki kwa kujitoa uhai katika Kituo cha Polisi cha Mai-A-Ihii huko Kikuyu.

Familia ya marehemu ilisema kuwa jamaa yao alikamatwa na kuzuiliwa katika kituo hicho Ijumaa usiku.

Mamake alipofika kituoni kumtazama mwanawe Jumamosi, hata hivyo alifahamishwa kuwa alijitoa uhai.

Kamanda wa Polisi wa Kikuyu Ronald Kirui alisema maafisa wa polisi waliokuwa zamu usiku wa kisa hicho walirekodi taarifa sawa.

"Mwili huo umehamishwa hadi katika chumba cha kuhifadhia maiti kilicho karibu ambapo uchunguzi wa maiti utafanywa ili kubaini chanzo hasa cha kifo cha marehemu," alisema.

Aliwataka wadau wote kuendelea kuwa wavumilivu wakati wa kuhitimisha uchunguzi wa tukio hilo.

Wenyeji walikuwa wamepinga kifo Jumamosi na kutaka hatua kwa waliohusika na tukio hilo.