logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Familia ya Kakamega yajawa majonzi baada ya ndugu wawili kufariki katika mzozo wa miti

Kisa hicho pia kiliwaacha wengine kadhaa wakiwa wamejeruhiwa, akiwemo afisa wa polisi.

image
na SAMUEL MAINA

Habari11 February 2024 - 05:57

Muhtasari


  • •Kisa hicho ambacho kilitokea katika kijiji cha Eregi, Ikolomani Mashariki pia kiliwaacha wengine kadhaa wakiwa wamejeruhiwa, akiwemo afisa wa polisi.
  • •Seneta wa Kakamega Boni Khalwale alisema kwenye taarifa kupitia X kwamba anaifahamu familia hiyo kibinafsi.
Wakaazi wakusanyika kuzunguka nyumba katika kijiji cha Eregi, Kaunti ya Kakamega baada ya vita vya miti kuzuka, Jumamosi, Februari 10, 2024.

Familia moja katika Kaunti ya Kakamega imeingia katika maombolezo baada ya ndugu wawili kufariki siku ya Jumamosi katika mzozo wa miti.

Kisa hicho ambacho kilitokea katika kijiji cha Eregi, Ikolomani Mashariki pia kiliwaacha wengine kadhaa wakiwa wamejeruhiwa, akiwemo afisa wa polisi.

Wakazi na wanafamilia walisema ndugu hao walianza kupigania haki ya kukata miti kwenye ardhi iliyoachwa na marehemu baba yao.

Walisema polisi wakijibu mzozo uliofuata walifyatua risasi kadhaa, na wakati kila kitu kiliponyamaza, ndugu hao wawili walikuwa wamekufa.

“Walikuja mbio na kuingia nyumbani kwangu, mmoja alikuwa ameshika panga na akaanza kumkata dada yao,” jirani mmoja alisema.

"Milio ya risasi ilisikika, sijui zilimpata aje mume wangu. Waliendelea kwa muda," mjane wa mmoja wa marehemu alisema.

Seneta wa Kakamega Boni Khalwale alisema kwenye taarifa kupitia X kwamba anaifahamu familia hiyo kibinafsi.

Alisema mmiliki wa shamba hilo marehemu Mzee Shisanya Angote alimuuzia sehemu yake baada ya kuigawanya na kuwagawia watoto wake wa kiume na wa kike.

Seneta huyo alisema alijenga polytechnic kwenye ardhi aliyonunua kutoka kwa mzee huyo baada ya kugawanywa.

“Inasikitisha sana kwamba wanawe wawili wamepoteza maisha huku wakiingilia kile ambacho baba yao alimpa dada yao, Madam Maureen Bunoro Shisany,” alisema.

Seneta huyo aliwatakia waliojeruhiwa katika ajali hiyo ahueni ya haraka na kuwataka wakazi na familia kudumisha amani huku vyombo vya usalama vikijitahidi kurejesha utulivu.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved