Mwanamke mwenye umri wa miaka 42 alidungwa kisu na kuuawa katika tukio la kustajabisha jijini Nairobi, polisi wamesema.
Maafisa wa upelelezi bado hawajakamata mshukiwa wa mauaji hayo, yaliyotokea katika mtaa wa mabanda wa Riruta siku ya Jumanne.
Polisi walisema walikuwa wakimsaka mwanamke ambaye anadaiwa kumdunga kisu mwingine katika ugomvi wa kufua nguo.
Walikuwa wamezozana kuhusu mahali pa kuanika nguo zao walizokuwa wamefua, polisi walisema.
Ugomvi huu uligeuka ndani ya dakika na kuwa makabiliano makali. Marehemu alitambulika kwa jina Stellah Syokau, mwenye umri wa miaka 42.
Maafisa wa usalama wanasema mshukiwa alichukuwa kisu cha jikoni na kumdunga marehemu mgongoni. Polisi walitembelea eneo la tukio na kupata kisu cha jikoni.
Mshukiwa alitoroka eneo la tukio na juhudi za kumtafuta zinaendelea, polisi walisema.
Polisi waliuhamisha mwili huo hadi chumba cha kuhifadhia maiti ukisubiri uchunguzi wa maiti.