Licha ya tume ya utumishi wa umma kujitenga na uteuzi wa Mwanahabari Jacque Maribe kama afisa mkuu wa mawasiliano katika wizara ya utumishi wa umma, mwanahabari huyo alionekana akiandamana na waziri wa Utumishi wa Umma Moses Kuria katika ziara ya kikazi.
Waziri Kuria alikuwa kwenye ziara ya kikazi katika kaunti ya Nakuru siku ya Alhamisi na Maribe alikuwa miongoni mwa watu ambao waliandamana na waziri.
Kuria alikuwa katika maeneo bunge mbalimbali mjini Nakuru siku ya mnamo Alhamisi. Mwanahabari huyo ambaye wiki chache zilizopita aliondolewa shtaka la mauaji alikuwa ameketi karibu na maafisa wa idara ya utumishi wa umma na karibu Kuria.
Ziara hiyo ilijiri saa chache baada ya Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) kukanusha habari kwamba Maribe amepata kazi katika Wizara ya Kuria. Ripoti zilidokeza hapo awali kuwa Waziri wa Utumishi wa Umma Moses Kuria alimteua Maribe kama mkuu wa mawasiliano katika afisi yake. I
Licha ya uteuzi huo kuhusishwa na Kuria, waziri alidai kwamba mambo ya kuajiri wafanyikazi wa serikali lilikuwa jukumu la tume ya PSC.
Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) ilipuuzilia mbali ripoti kwamba wamemteua aliyekuwa mwanahabari Jacque Maribe katika Wizara ya Utumishi wa Umma, kuwa afisa mkuu wa Mawasiliano.
Katika taarifa Machi 14 Alhamisi, mwenyekiti wa PSC Anthony Muchiri alisisitiza kuwa hakuna uteuzi kama huo ambao umefanywa na bodi haijapokea ombi lolote la kuajiri Maribe.
"Kwa rekodi, nafasi iliyotajwa itajazwa kupitia mchakato wa kuajiri wenye ushindani iwapo nafasi itatokea," alisema Muchiri.