Kaunti ya Taita Taveta yafuta ada za matibabu za wanafunzi wa KU

Majeruhi 18 wametibiwa na kuruhusiwa kujiunga na familia zao , nayo mili ya wanafunzi 11 ikihifadhiwa katika makafani ya hospitali ya Moi mjini Voi

Muhtasari

• Wanafunzi hao walilazwa katika hospitali ya Voi siku ya Jumatatu.

• Basi walimokuwa wakisafiria lilihusika katika ajali ya barabarani eneo la Maungu, barabara kuu ya Nairobi-Mombasa.

Maafisa wa matibabu wakihamisha mhasiriwa wa ajali iliyohusisha basi la Chuo Kikuu Cha Kenyatta kutoka kwa matibabu zaidi kutoka Voi.
Maafisa wa matibabu wakihamisha mhasiriwa wa ajali iliyohusisha basi la Chuo Kikuu Cha Kenyatta kutoka kwa matibabu zaidi kutoka Voi.
Image: SOLOMON MUINGI

Serikali ya kaunti ya Taita Taveta imetangaza kufutilia mbali gharama zote za matibabu kwa wanafunzi 42 wa chuo kikuu cha Kenyatta.

Wanafunzi hao walikimbizwa katika hospitali hiyo siku ya Jumatatu baada ya basi walimokuwa wakisafiria kuhusika katika ajali ya barabarani eneo la Maungu, barabara kuu ya Nairobi-Mombasa.

Akizungumza alipowatembelea wajeruhi katika hospitali ya Rufaa ya Moi mjini Voi,  Gavana  wa kaunti hiyo Andrew Mwadime alipongeza juhudi za madaktari, wauguzi na wote waliohusika kutoa huduma za matibabu kwa wanafunzi hao.

Ajali hiyo ilisababisha vifo vya wanafunzi 11 waliokuwa katika safari ya masomo. Basi walimokuwa wakisafiria liligongana na trela.

Aidha gavana Mwadime alituma risala za rambi rambi kwa familia ya wanafunzi waliofariki kutokana na ajali hiyo , akiwataka madereva kuwa waangalifu wanapokuwa barabarani.

Ripoti ya madaktari imeeleza kuwa kati ya majeruhi  24, 18 wamefanikiwa kutibiwa na kuruhusiwa kujiunga na familia zao , nayo mili ya wanafunzi 11ikihifadhiwa katika makafani ya hospitali iyo hiyo. 

Juhudi za chuo hicho kuwasafirisha wanafunzi hao hadi jijini Nairobi kwa matibabu zaidi zimekuwa zikiendelea.