Mwanafunzi aliyenusurika kifo kwenye ajali ya basi la Chuo cha Kenyatta afichua kilichotokea

Alisema dereva wa basi lalikuwa akijaribu kuyapita magari mengine wakati tukio hilo la kusikitisha lilipotokea.

Muhtasari

•Onyango alisema walikuwa wamesogea umbali wa kilomita kadhaa tu kupita Mtito Andei ajali hiyo ilipotokea mwendo wa saa moja jioni.

•Alisema kuwa watu waliokaa upande wa nyuma wa basi la shule waliumia zaidi kwani ndipo palipokuwa na athari kubwa.

lililohusika katika ajali.
Basi lililohusika katika ajali.
Image: HISANI

Mwanafunzi mmoja aliyenusurika katika ajali mbaya ya barabarani iliyoua wanafunzi kadhaa wa Chuo Kikuu cha Kenyatta na kuwaacha wengine na majeraha amefichua kuwa dereva wa basi lao alikuwa akijaribu kuyapita magari mengine wakati tukio hilo la kusikitisha lilipotokea.

Akizungumza na Daily Nation, Felix Onyango alisema walikuwa wamesogea umbali wa kilomita kadhaa tu kupita Mtito Andei ajali hiyo ilipotokea mwendo wa saa moja jioni.

Alisema dereva wao alikuwa akijaribu kurudi kwenye njia yake wakati trela iliyokuwa ikija ilipogonga upande wa nyuma wa basi la shule.

“Dere alikuwa anaovertake, gari ilikuwa refu kuovertake. Wale wasee wa nyuma wakagongwa na trela,” mwanafunzi huyo alisimulia.

Onyango alisema kuwa watu waliokaa upande wa nyuma wa basi la shule waliumia zaidi kwani ndipo palipokuwa na athari kubwa kutokana na ajali hiyo.

Pia alifichua kuwa yeye na wenzake wengine ambao hawakuwa wamefunga mkanda wa usalama walitupwa nje ya basi kutokana na athari ya ajali.

“Watu wenye walikuwa nyuma ndio waliumia sana. Sisi wenye hatukuwa tumefunga mshipi tukatupwa nje. Mimi nimeumia mkono pekee yake. Mwenzangu huyu aliumia shingo. Wengine walitupwa nje sasa sijui mahali,” alisema.

Mwanafunzi huyo alisema basi hilo lilipoteza mwelekeo baada ya kugongwa na kuwatupa nje baadhi ya wanafunzi.

Hata hivyo, alipoteza fahamu baada ya ajali hiyo na akapata ufahamu tena walipokuwa wakiokolewa.

Takriban wanafunzi 11 wa Chuo Kikuu cha Kenyatta walifariki Jumatatu jioni katika ajali mbaya ya barabarani iliyohusisha basi lao la shule na trela, Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Voi Ibrahim Daffala alithibitisha.

Daffala alisema wanafunzi 10 walifariki papo hapo huku mwingine akikata roho hospitalini.

Wanafunzi 42 walipata majeraha mabaya huku wanne wakiwa na majeraha madogo.

"Ajali hiyo ilitokea wakati mvua kubwa ilikuwa ikinyesha. Lori lilijaribu kuondoka kutoka barabarani ili kuepuka mgongano wa uso kwa uso na kusababisha ajali," Daffala alisema.

Picha zilizofikia Radio Jambo zinaonyesha basi la shule liligongwa upande wa kushoto.