Mcheza santuri maarufu wa Kenya Joseph Mwenda almaarufu DJ Joe Mfalme ametoa taarifa baada ya kukamatwa kuhusiana na kifo cha afisa mkuu wa polisi.
DJ Joe Mfalme alikamatwa wikendi, pamoja na mlinzi wake, dereva na mpiga picha kuhusiana na madai ya kushambuliwa kwa mpelelezi wa Kituo cha Polisi cha Kabete Felix Kelian ambaye baadaye alifariki dunia Ijumaa Machi 22. Pia wanaohojiwa ni maafisa watatu wa polisi walioshughulikia ajali hiyo ambapo madai ya shambulio hilo yalitokea.
Katika taarifa yake Jumapili jioni, DJ huyo alisema kuwa yeye na timu yake wamekuwa wakishirikiana vyema na maafisa wa uchunguzi tangu tukio hilo litokee Machi 16, 2024.
"Kwanza kabisa, tunatoa pole kwa familia, marafiki na wote walioguswa na tukio hili la kusikitisha," DJ Joe Mfalme alisema katika taarifa yake.
Aliongeza, “DJ Joe Mfalme na timu yake wamekuwa kwa ushirikiano wa karibu na vyombo vya uchunguzi tangu kutokea kwa tukio hilo. DJ Joe Mfalme na timu yake wamejizatiti kikamilifu kushiriki katika utaratibu wa uchunguzi na wataendelea kutoa ushirikiano wao kadri itakavyohitajika."
Mtumbuizaji huyo pia ameeleza matumaini yake kwamba uchunguzi wa uwazi na wa haki utafanywa, na ukweli utafichuliwa.
Lakini huku akibainisha unyeti wa suala hilo, alisema hatazungumzia zaidi suala hilo.
"Kwa mara nyingine tena, tunatuma risala zetu za rambirambi kwa familia na marafiki waliofiwa na msiba huu," alisema.
"Kwa kuzingatia uchunguzi unaoendelea na hali nyeti ya suala hilo, tutajizuia kutoa taarifa zaidi kwa wakati huu. Tutakusudia kukupa taarifa mara tu uchunguzi utakapokamilika."
Mnamo Machi 16, DJ Mfalme na timu yake walikuwa wakielekea nyumbani Kikuyu walipohusika katika ajali ndogo isiyo ya majeraha.
Polisi walisema gari lake lilikwaruzwa katika ajali hiyo.
Hii ilisababisha ugomvi na Kelian kabla ya polisi kuitwa kwenye eneo la tukio.
Maafisa hao walimpeleka Kelian kituoni ambako alianza kulalamika maumivu ya tumbo. Pia alianza kukojoa damu, mashuhuda walisema.
Baadaye afisa huyo alipelekwa hospitalini ambako alifanyiwa upasuaji lakini alifariki Ijumaa, Machi 22, alipokuwa akipokea matibabu katika Hospitali ya Nairobi West.
Polisi walisema wanachunguza mauaji katika tukio hilo.