Maisha yangu yako hatarini - Mbunge Wamboka adai kabla ya hoja dhidi ya Linturi

"Nimefuatwa na magari yasiyo na nambari za usajili na watu wasiojulikana; si rahisi lakini nitapigania uadilifu wa Jamhuri ya Kenya," Wamboka alisema.

Muhtasari

• Kamati maalum ya bunge ya wanchama 11 ambayo inashughulikia hoja ya kuondolewa kwa CS Linturi itaendesha vikao vya siku tatu mfululizo kuanzia Jumatano hadi Ijumaa.

Wakili John Khaminwa akiwa na mteja wake Mbunge wa Bumula Jack Wamboka Wanami wakiwasili katika majengo ya bunge mnamo Mei.7.2024/EZEKIEL AMINGÁ
Wakili John Khaminwa akiwa na mteja wake Mbunge wa Bumula Jack Wamboka Wanami wakiwasili katika majengo ya bunge mnamo Mei.7.2024/EZEKIEL AMINGÁ

Mbunge wa Bumula Jack Wamboka Wanami ambaye ndiye mwenye hoja ya kumtimua waziri wa Kilimo Mithika Linturi sasa anadai maisha yake yako hatarini.

Wambokja mnamo siku ya Jumanne aliambia kamati maalum inayochunguza madai yaliyotolewa dhidi ya CS linturi kuwa amekumbwa na matukio ya kutiliwa shaka ambayo alihusisha na ombi lake la kutaka Linturi ang'atuke ofisini.

"Nimefuatwa na magari yasiyo na nambari za usajili na watu wasiojulikana; si rahisi lakini nitapigania uadilifu wa Jamhuri ya Kenya," Wamboka alisema.

Aliwataka wabunge  wanachama wa kamati hiyo kuimarisha usalama wa wabunge katika mazingira hayo.

Akizungumza katika majengo ya Bunge siku ya Jumanne, Wamboka alionyesha imani kuwa ana ushahidi wa kutosha kumtuma waziri Linturi nyumbani.

"Tumewasilisha ushahidi wetu. Tuko tayari kwa kesi. Tuko tayari kudhihirishia ulimwengu mzima kwamba Mithika Linturi ametenda kinyume na Katiba,” akasema.

Mbunge huyo aliandamana na wakili wake John Khaminwa.

Wamboka alishikilia ombi lake la kumwondoa Linturi afisini kwa makosa matatu, ambayo ni ukiukaji mkubwa wa Katiba au sheria nyingine yoyote, sababu kuu za kuamini kuwa Waziri Mkuu ametenda uhalifu chini ya sheria za kitaifa, pamoja na utovu wa nidhamu mkubwa.

Kamati maalum ya bunge ya wanchama 11 ambayo inashughulikia hoja ya kuondolewa kwa CS Linturi itaendesha vikao vya siku tatu mfululizo kuanzia Jumatano hadi Ijumaa.

Wa kwanza kufika mbele ya kamati hiyo siku ya Jumatano ni mfadhili wa hoja hiyo mbunge Wamboka Wanami.

Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula tayari amewaita wabunge kwa kikao maalum Jumatatu kujadili ripoti ya kamati hiyo.

“Kwamba, kwa mujibu wa masharti ya Ibara ya 152 (7) (b) ya Katiba na Kanuni za Kudumu za 64(3) na 66, nimeteua Jumatatu, tarehe 13 Mei 2024 saa 8.30 alasiri  kuwa siku na muda wa kikao maalum cha Bunge. Bunge kupokea ripoti ya Kamati maalum,” mawasiliano kutoka kwa Spika yalisomeka.

Wabunge walienda kwa mapumziko marefu Mei 2 na wamepangwa kurejelea vikao Juni 4.

Wetang'ula alimwagiza Karani wa bunge kuhakikisha wabunge wote wamepata ujumbe huu.

Imetafsiriwa na Davis Ojiambo.