Kijana mkimbizi auawa kwa kisu baada ya mapigano kuzuka wakati wa mechi ya soka Kakuma

Hili limewafanya maafisa kukagua hatua mbalimbali za usalama katika kituo hicho.

Muhtasari

•Maah Kim Lat mmoja, 22 ambaye ni mkimbizi na mkazi wa kambi ya wakimbizi ya Kakuma Four alidungwa kisu tumboni.

•Hakuna aliyekamatwa lakini polisi walisema wanachunguza suala hilo.

Crime scene
Crime scene
Image: HISANI

Maafisa wa upelelezi wanachunguza kisa ambapo mkimbizi wa Sudan Kusini alidungwa kisu na kuuawa katika mapigano kwenye kambi ya wakimbizi ya Kakuma, Kaunti ya Turkana.

Hii ilitokea wakati wa mechi ya kandanda kati ya kundi la vijana wa Nuer ambao ni wakimbizi huko, polisi walisema.

Polisi walisema tukio hilo lilitokea Mei 17.

Hili limewafanya maafisa kukagua hatua mbalimbali za usalama katika kituo hicho.

Kulingana na polisi, kundi hilo lilitofautiana na kujihusisha katika mzozo huo huku mawe na matawi yakitanda hewani.

Hapo ndipo Maah Kim Lat mmoja, 22 ambaye ni mkimbizi na mkazi wa kambi ya wakimbizi ya Kakuma Four alipodungwa kisu tumboni.

Polisi walisema alikimbizwa katika Hospitali ya Clinic Seven, ambapo alifariki dunia kutokana na majeraha alipokuwa akipatiwa matibabu.

Hakuna aliyekamatwa lakini polisi walisema wanachunguza suala hilo.

Polisi walisema wanafanya mipango kadhaa ya usalama ili kuhakikisha usalama wa wakimbizi huko.

Hii inafuatia msururu wa visa vya vifo vinavyoripotiwa katika kambi hiyo.

Ni pamoja na mashambulizi ya kulipiza kisasi ambapo hata bunduki zimetumika katika Kambi ya Wakimbizi ya Kakuma na Makazi Jumuishi ya Kalobeyei.

Kambi ya Kakuma imegawanywa katika maeneo manne: Kakuma 1, 2, 3 na 4 wakati Makazi Jumuishi ya Kalobeyei yanajumuisha vijiji vitatu.

Kambi ya Wakimbizi ya Kakuma iko katika Kaunti ya Turkana na ilianzishwa mwaka wa 1992 kufuatia kuwasili kwa "Lost Boys of Sudan".

Mashirika mbalimbali yanaisaidia kambi hiyo kwa njia nyingi.

Utafsiri: Samuel Maina