logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Mwanafunzi wa kidato cha tatu, Baringo aliuawa kwa kuteswa, Uchunguzi wabaini

Kabla ya kifo chake, mwanafunzi huyo alipata matatizo katika mapafu.

image
na Radio Jambo

Yanayojiri22 May 2024 - 13:26

Muhtasari


• Mwanapatholojia wa serikali Benson Macharia alisema mwanafunzi huyo alipata majeraha mabaya ambayo pia yalisababisha kuvuja damu nyingi.

Mwanapatholojia Dkt Benson Macharia akizungumza katika Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Moi (MTRH) mjini Eldoret Mei 21 2024.

Mwanafunzi wa kidato cha tatu mwenye umri wa miaka 19 anayedaiwa kuuawa na Askari wa msitu katika Kaunti ya Baringo aliteswa vikali kabla ya kifo chake, uchunguzi wa maiti yake umebaini.

Uchunguzi wa upasuaji wa maiti uliofanywa na Mwanapatholojia wa serikali Benson Macharia katika Hospitali ya Rufaa ya Moi huko Eldoret ulifichua kuwa Stephen Mwangi alifariki kutokana na majeraha mengi ya tishu laini yaliyosababishwa na kifaa butu.

‘Majeraha yalikuwa juu ya mwili wake kuanzia nyonga hadi mgongoni na sehemu nyingine za mwili”, alisema Dkt Macharia.

Dkt Macharia ambaye alitekeleza zoezi la uchunguzi wa maiti mbele ya familia na polisi alisema mwanafunzi huyo alipata majeraha hayo ambayo pia yalisababisha kuvuja damu nyingi.

"Pia kulikuwa na majeraha kwenye mikono ambayo yanaweza kuwa dalili kwamba alijaribu kujikinga," alisema Dk Machari.

Aidha alifichua kuwa kabla ya kifo chake, mwanafunzi huyo alipata matatizo katika mapafu kwa kile kinachojulikana kitabibu kama ugumu wa kupumua (respiratory distress syndrome).

Mwanapatholojia huyo alikuwa akizungumza na vyombo vya habari baada ya kufanya uchunguzi wa mwili wa marehemu katika chumba cha kuhifadhi maiti cha MTRH kaunti ya Uasin Gishu.

 Aliandamana na wanafamilia wa mwanafunzi aliyeuawa wakiongozwa na mamake Mary Wambui.

"Ni dhahiri kwamba mwanangu aliteswa vibaya lakini ninamwachia Mungu kila kitu hata tunapojiandaa kumzika", alisema Wambui.

Mwanafunzi huyo aliaga dunia wiki jana alipokuwa akipokea matibabu katika kitengo cha wagonjwa mahututi cha Hospitali ya Rufaa ya Moi ambako alikuwa amekimbizwa baada ya kisa hicho kinachodaiwa.

Kifo cha Mwangi kilitokea wakati wa makabiliano na maafisa wa Huduma za Misitu nchini (KFS). Ilisemekana alikuwa akijaribu kuwazuia maafisa dhidi ya kumnyanyasa kingono mamake katika msitu wa Koibatek.

Kulingana na mamake marehemu, kosa pekee la mwanawe lilikuwa kuingilia kati kujaribu kumwokoa alipokuwa akiteswa na maafisa wanaolinda msitu wa umma.



RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved