Rais William Ruto amejitokeza kutetea chaguo lake la kukodisha ndege ya kibinafsi kusafiri wakati wa ziara yake ya hivi majuzi nchini Marekani.
Hii ni baada ya ukosoaji mwingi kutoka kwa umma huku kundi la wakosoaji wakishangaa kwa nini hangetumia ndege rasmi ya rais ama ndege la shirika la ndege la Kenya Airways.
Katika taarifa yake siku ya Jumapili, rais Ruto aliwahakikishia Wakenya kwamba gharama ya ndege ya kibinafsi aliyokodi ni nafuu kuliko kiasi ambacho kingetumiwa ikiwa angetumia ndege ya KQ.
“Wakenya wenzangu, nimeona wasiwasi kuhusu chombo changu cha usafiri hadi Marekani. Kama msimamizi anayewajibika wa rasilimali za umma na kulingana na azimio langu kwetu kuishi kulingana na uwezo wetu na kwamba ninafaa kuongoza kutoka mbele kwa kufanya hivyo, gharama ilikuwa ndogo kuliko kusafiri kwa KQ,” Ruto alisema kupitia akaunti yake rasmi ya Twitter.
Rais alisafiri kwenda Merika kwa ndege ya kifalme ya A6-RJU.
Ripoti nyingi zinakadiria kuwa gharama ya kukodisha ndege ya biashara ya Boeing kama ile ambayo Ruto alitumia katika ziara yake Marekani ni karibu $18,000 kwa saa, takriban Sh2,358,0000.
Safari ya kuelekea Atlanta, Marekani, ambako Ruto alisimama kwa mara ya kwanza, ni takriban saa 19 kutoka Kenya, kumaanisha kwamba ingegharimu Sh71,404,500 kwa kiwango hicho.
Hapo awali, ubalozi wa Marekani ulikana kulipa gharama za usafiri za Rais Ruto hadi Marekani.
"Ili tu kuwa wazi: Marekani HAIKULIPIA ndege ya Rais Ruto kwenda Marekani," Msemaji wa Ubalozi wa Marekani jijini Nairobi Andrew Veveiros aliambia shirika la habari la ndani.