Jamaa afungwa jela miaka 2 kwa kuchoma picha ya rais

Chuala alitumwa gerezani kutumikia kifungo cha miaka miwili au kulipa faini ya shilingi milioni tano.

Muhtasari

•Chaula aliaguizwa kutumikia kifungo cha miaka miwili (2) gerezani au kulipa faini ya shilingi millioni 5 pesa za Tanzania (Ksh242,000).

•Mshtakiwa huyo hata hivyo aliepelekwa gerezani kwenda kutumikia kifungo baada ya kushindwa kulipa faini.

Mshtakiwa Shedrack Yusuph Chaula
Image: HISANI

Jamaa mmoja kutoka Tanzania ambaye alijerekodi akimkashifu rais Samia Suluhu Hassan na hadi kuchoma picha yake amehukumiwa kifungo cha jela.

Siku ya Alhamisi, Julai 4, 2024, mahakama ya wilaya ya Rungwe ilimtia hatiani Bw. Shedrack Yusuph Chaula kutumikia kifungo cha miaka miwili (2) gerezani au kulipa faini ya shilingi millioni 5 pesa za Tanzania (Ksh242,000) kwa kosa la kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni kwa mujibu wa kifungu cha 16 cha sheria ya makosa ya mtandaoni 2015.

Huku akisoma hati ya mashtaka mbele ya hakimu mkazi mkuu wa mahakama ya wilaya ya Rungwe Mh. Ramla Shehagiro, mwendesha mashtaka wa serikali Rosemary Mgeniji alieleza kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo mnamo 22/6/2024 katika kijiji cha Ntokela wilayani Rungwe mkoani Mbeya.

Mahakama iliambiwa na mwendesha mashtaka kuwa mshtakiwa huyo akiwa dukani kwake maeneo ya Ntokela alirekodi ujumbe wa video wenye maneno; “Kwakua umeshindwa kutetea taifa lako lisiathirike na ushoga hii video inakuhusu wewe na si mtu mwingine” huku akijua kuwa taarifa hizo ni za uongo zenye kupotosha jamii.

Jamaa huyo mwenye umri wa miaka 24 alipopewa nafasi ya kujitetea mahakamani hapo mtuhumiwa huyo Bw. Shadrack Chaula mkazi wa Ntokela amesema yupo tayari kutumikia adhabu yoyote atakayopewa na mahakama hiyo.

Upande wa serikali ukiongozwa na mawakili wa serikali Veronica Mtafya na Rosemary Mgeniji umeiomba mahakama itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine kwani kitendo hicho kimetafsiriwa kama udhalilishaji kwa Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wakati akitoa hukumu hakimu mkazi mkuu wa mahakama ya wilaya ya Rungwe Ramla Shehagiro amesema kwa mujibu wa sheria ya makosa ya mtandao ya mwaka 2015 kifungu cha 16 amemtia hatiani kwenda gerezani kutumikia kifungo cha miaka miwili au kulipa faini ya shilingi milioni tano.

Mshtakiwa huyo hata hivyo aliepelekwa gerezani kwenda kutumikia kifungo baada ya kushindwa kulipa faini.