"Hii ndiyo aina ya serikali tunayohitaji!- Atwoli asema kuhusu baraza mpya la mawaziri

Huku akiangazia umahiri wa walioteuliwa, Atwoli alisisitiza kuwa hakuna suala la upinzani kushirikiana na Rais.

Muhtasari

•Atwoli aliwataka Wakenya kuamini chaguo la Rais kwa uthabiti wa nchi na kuongeza kuwa ubora wa walioteuliwa ni wa juu.

•Atwoli alisema Rais anafaa kuwateua vijana katika nyadhifa zilizosalia.

ATWOLI
ATWOLI
Image: ATWOLI//X

Katibu mkuu wa Cotu Francis Atwoli ameunga mkono uteuzi wa Rais William Ruto wa wanachama wa ODM katika baraza lake la mawaziri.

Huku akiangazia umahiri wao, Atwoli alisisitiza kuwa hakuna suala la upinzani kushirikiana na Rais.

Akizungumza mjini Kisumu siku ya Jumamosi, Atwoli aliwataka Wakenya kuamini chaguo la Rais kwa uthabiti wa nchi na kuongeza kuwa ubora wa walioteuliwa ni wa juu.

"Hii ndiyo aina ya serikali tunayohitaji," alisema.

Mnamo Jumatano, Ruto alijumuisha wanachama wanne wa ODM katika baraza lake jipya la mawaziri na kumpa mbunge mteule John Mbadi wizara kuu ya Hazina ya Kitaifa.

Pia alimteua aliyekuwa Gavana wa Mombasa Hassan Joho kuongoza wizara ya Madini na Uchumi wa Majini

Aliyekuwa gavana wa Kakamega na naibu kiongozi wa ODM Wycliffe Oparanya aliteuliwa katika Wizara ya Vyama vya Ushirika na Maendeleo ya MSME huku Mbunge wa Ugunja na kiongozi wa wachache katika Bunge la Kitaifa Opiyo Wandayi akikabidhiwa Wizara ya Nishati na Petroli.

Ruto, hata hivyo, bado hajawataja waliopendekezwa katika afisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wizara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na ASAL.

Atwoli alisema Rais anafaa kuwateua vijana katika nyadhifa zilizosalia.

Aliongeza kuwa ikiwa Rais na kinara wa ODM Raila Odinga wangeamua kuwa baadhi ya watu kutoka Azimio wanafaa kuchangia utulivu wa nchi basi hayuko katika nafasi ya kubishana nayo.

Mwanaharakati huyo wa vyama vya wafanyikazi alimtetea Raila kutokana na hasira za wakosoaji ambao wamemkashifu kwa kuwaruhusu wanachama wa chama chake kujiunga na baraza la mawaziri la Ruto.

Atwoli alidai kuwa Raila amekuwa akitenda kwa manufaa ya Wakenya mara kwa mara.

“Raila hajawahi kuwatelekeza Wakenya, uhuru tunaofurahia leo ulivaliwa na juhudi zake kwa sababu alijitolea pakubwa kwa ajili ya nchi hii na kujitolea kwake huko nyuma kunastahili kutambuliwa,” aliambia vyombo vya habari.

"Wale waliokuwa wakimkosoa Raila walikuwa wapi alipopigania uhuru huu? Yeye na familia yake wamevumilia mengi. Ni wakati wa kumtuza," Atwoli aliongeza.

Aidha alithibitisha kuunga mkono kwa Cotu kwa kozi ya Gen Z na kuwasifu Wakenya vijana kwa uanaharakati wao.