Kenya Power inatarajia kuunganisha kaya 9,121 katika kaunti nne kwa gridi ya taifa baada ya kupata shilingi 1.85 bilioni kutoka Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japani (JICA).
Kwenye Awamu ya V ya Mradi wa Last Mile Connectivity (LMCP), msaada huu utafadhili uunganishaji wa umeme katika kaunti za Nakuru, Kilifi, Kwale na Nyandarua ambapo JICA inafadhili miradi mingine muhimu ya nishati.
“Tuna matarajio ya kuunganisha kaya zote zilizokusudiwa katika kaunti hizi nne kufikia Januari 2025.
Kampuni inajitahidi kwa hali ya juu kuhakikisha uunganishaji wa umeme unaendelea kwa kasi katika nchi nzima ili kufanikisha upatikanaji wa umeme kwa kila mmoja,” alisema Rosemary Oduor, Meneja Mkuu wa Huduma za Kibiashara na Mauzo wa Kenya Power.
Msaada huu kutoka Japan umetolewa miezi miwili baada ya Kenya Power kutia sahihi mikataba ishirini na sita kwa ajili ya utekelezaji wa Awamu ya IV ya LMCP.
“Tunashukuru JICA kwa msaada huu ambao utasaidia sana kaya hizi kupata umeme na kubadilisha maisha yao,” aliongeza Oduor.
Awamu IV ya mradi huu inafadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Umoja wa Ulaya (EU) na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) kwa jumla ya shilingi bilioni 27 na itawaunganisha wateja wapya 280,000 kwa gridi ifikapo Novemba 2025.
Kenya Power inasema kuwa imepiga hatua kubwa kwa kutumia shilingi bilioni 73.1 hadi sasa katika mradi huu unaotegemea Mkakati wa Kitaifa wa Umeme wa Kenya ulioandaliwa mwaka 2015 ili kuboresha upatikanaji wa umeme nchini.
Mradi huu umeweza kuongeza kiwango cha upatikanaji wa umeme nchini Kenya hadi asilimia 76 ya idadi ya watu huku kaya 9.6 milioni zikihusishwa na gridi.
Jumla ya kaya 746,867 zimeunganishwa na gridi chini ya awamu tatu za kwanza kwa gharama ya shilingi bilioni 51.1.