Rais Ruto akana madai ya kuungana na ODM

Rais alipongeza ODM kwa kukubali kufanya kazi na serikali kwa minajili ya kusukuma mbele ajenda ya maendeleo ya nchi.

Muhtasari

• Rais William Ruto alisema mirengo hiyo miwili ya kisiasa imekubaliana kushirikiana ili kusaidia kukabiliana na changamoto zinazowakumba Wakenya.

Ruto na Raila waonesha nia ya kupatana.
HANDSHAKE Ruto na Raila waonesha nia ya kupatana.
Image: Facebook

Muungano wa Kenya Kwanza na ODM hawaijaingia katika makubaliano ya kuungana bali wameafikiana tu kuunganisha nchi na kuwatumikia Wakenya.

Rais William Ruto alisema mirengo hiyo miwili ya kisiasa imekubaliana kushirikiana ili kusaidia kukabiliana na changamoto zinazowakumba Wakenya.

Alisema mpangilio huo hauongozwi na masilahi ya kibinafsi au ya kisiasa bali ni kwa manufaa ya watu wa Kenya.

"Inafika wakati jambo muhimu zaidi si kile ambacho kinanufaisha viongozi au vyama vya siasa, lakini kile ambacho kinawanufaisha wananchi," alisema.

Akizungumza katika kaunti za Nyamira na Kisii katika siku yake ya kwanza ya ziara ya maendeleo ya siku tatu rais alibainisha kuwa kazi yake kuu ni kuunganisha nchi.

Alikuwa ameandamana na Naibu Rais Rigathi Gachagua, Magavana Simba Arati (Kisii) na Amos Nyaribo (Nyamira), Waziri wa mpya wa Elimu Julius Ogamba, wabunge na wawakilishi wadi.

Rais alipongeza ODM kwa kukubali kufanya kazi na serikali kwa minajili ya kusukuma mbele ajenda ya maendeleo ya nchi.

Aliwataka maafisa wakuu wa serikali, Wabunge na Mahakama kufanya kazi kwa amani kwa faida na manufaa ya taifa la Kenya.

Aliwataka Wakenya kuunga mkono serikali pana kwa ajili ya umoja wa kitaifa.

Aliwataka viongozi wote wakiwemo kutoka Gusiiland kuweka kando tofauti zao za kisiasa na kufanya kazi pamoja kuwatumikia wananchi.

"Ninawaomba tuungane ili tuwe na nguvu ya kupeleka Nyamira, Kisii na Kenya mbele," alisema.

Kuhusu maendeleo, Rais Ruto alisema serikali inaboresha vifaa katika shule 68 katika maeneo bunge ya Borabu, Mugirango Kaskazini, Mugirango Magharibi na Kitutu Masaba kaunti ya Nyamira.

Katika Eneo Bunge la Mugirango Kaskazini, rais aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa bweni katika Shule ya Upili ya Kiabonyoru.

Pia aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la kusomea katika Shule ya Msingi na Sekondary ya msingi ya Kenyerere katika eneo bunge la Kitutu Masaba.

Baadaye, alizindua mradi wa usambazaji wa umeme katika kijiji cha Nyang’eni huko Nyaribari Chache, Kaunti ya Kisii.