Kenya imekana kuhusika na madai ya kutekwa nyara kwa kiongozi wa upinzani nchini Uganda Kizza Besigye.
Katibu wa kudumu wa Masuala ya Kigeni Sing’oei Korir alisema Kenya haina jukumu lolote katika madai ya kukamatwa au kusafirishwa kwa Besigye.
"Hakuna sababu yoyote kwa Kenya kuwa mshirika katika kukamatwa kwake, ikiwa ipo," Korir alisema Jumatano.
"Sivyo kabisa! Ni upumbavu hata kudhani hivyo."
Besigye ameshindana na Rais wa Uganda Yoweri Museveni katika chaguzi nne na kushindwa kila mara, ingawa amekuwa akikataa matokeo.
Siku ya Jumatano, mke wa Besigye, Winnie Byanyima, alidai mumewe alikuwa ametekwa nyara jijini Nairobi siku ya Jumamosi katika eneo la Riverside Drive.
Kulingana na familia yake, Besigye alitekwa nyara jijini Nairobi na kupelekwa Uganda, ambako wanajeshi wanadaiwa kumzuilia.
"Naiomba serikali ya Uganda kumwachilia mume wangu Dr Kizza Besigye kutoka mahali anakozuiliwa mara moja. Alitekwa nyara Jumamosi iliyopita akiwa Nairobi kwa ajili ya uzinduzi wa kitabu cha Mh. Martha Karua. Sasa nina taarifa za uhakika kuwa yuko chini ya ulinzi wa jeshini mjini Kampala. Sisi familia yake na mawakili wake tunadai kumuona, yeye si mwanajeshi”, Byanyima alichapisha kwenye X.
Byanyima ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa Mpango wa Pamoja wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na VVU/UKIMWI (UNAIDS), Jumatano, aliliomba jeshi la Uganda kumwachilia Besigye kutoka kizuizi cha kijeshi huko Kampala ambako anaripotiwa kuzuiliwa.
Besigye alipatikana katika kizuizi cha kijeshi baada ya kutoweka Nairobi Jumamosi, Novemba 16.
Kutoweka kwake kunafuatia kukamatwa kwa wanaharakati 36 wa Uganda Julai 23 wanaohusishwa naye mjini Kisumu kabla ya kusafirishwa hadi Uganda.
Wanaharakati hao wa kisiasa walitekwa nyara na kusafirishwa hadi Uganda ambako walifunguliwa mashtaka ya uhaini na kupelekwa katika Gereza la Kitalya.
Wanaharakati hao ambao waliachiliwa kwa dhamana hivi majuzi, walikana mashtaka hayo na kusema walikuwa wakihudhuria warsha walipokamatwa.