Seneta wa kaunti ya Kericho Aaron Cheruiyot amemkosoa Askofu wa kanisa Katoliki jimbo la Nairobi Philip Anyolo kuwa ‘sheria’ aliyoitaja kwenye taarifa yake ya kukataa michango ya rais na gavana wa Nairobi bado haijafanywa rasmi kuwa sheria.
Kwa mujibu wa seneta huyo, sheria hiyo bado ni mswada na ipo katika hatua ya kujadiliwa kwenye bunge la seneti na kwamba haijafanywa kuwa sheria.
Kwenye mtandao wake wa X, seneta Cheruiyot amesema kuwa Wakenya wengi kwenye mitandao ya kijamii wanaunga mkono marufuku ya wanasiasa kuchangisha pesa katika makanisa ilhali wakati seneti lilihitaji maoni ya wananchi kuhusu mswada huo, viongozi wa kidini hawakutuma maoni yao.
Seneta Aaron Cheruiyot amesema kuwa asilimia 90 ya maoni yaliyotumwa kwenye bunge hilo, yalitaka kifungu cha 10 kwenye mswada huo kuondolewa kabisa. Kifungu hicho kinanuia kuzuia viongozi katika serikali na umma kutoshiriki katika hafla za kuchangisha fedha.
“Viongozi wetu wa kidini hawakutuma maoni yao kuhusu mswada huo.” Alisema seneta Aaron Cheruiyot.
Joto la uwajibishaji baina ya serikali na viongozi wa kidini linazidi kupamba moto mseto wa maoni kutoka kwa washikadau mbali mbali yakitolewa.
Usimamizi wa kanisa Katoliki lilikataa mchango kutoka kwa
rais William Ruto aliotoa katika kanisa Katoliki la Soweto jijini Nairobi siku
ya Jumapili. Rais, mnamo Jumapili alitoa mchango wa shilingi laki sita kwa
kwaya ya kanisa hilo huku gavana wa Nairobi Johnson Sakaja akitoa shilingi laki
mbili. Vile vile, Rais, William Ruto alitoa shilingi milioni 2 ya kufanikisha
ujenzi wa nyumba ya padre wa Parokia, pia akiahidi mchango mwingine wa shilingi
milioni 3 ya kununua basi la Parokia la Soweto.