
Gavana wa kaunti ya Kirinyaga Anne Waiguru amekuwa kiongozi wa hivi punde kushinikiza asasi za usalama kuhakikisha kuwa mshukiwa wa unyanyasaji wa kiijinsia katika kaunti ya Nakuru anakamatwa na kufikishwa mahakani ili haki ipatikane kwa kitendo cha unyama alichotekeleza.
Kupitia ukurasa wake wa X, gavana Waiguru amekashifu tukio hilo akisema kuwa kuna njia mwafaka za kusuluhisha mizozano ya kinyumbani bila ya vurugu akisisitiza kuwa ukatili wa kijinsia hauna nafasi katika jamii.
“Nalaani kisa cha kusikitisha huko Nakuru, ambapo mwanamume alimvamia mkwewe katika mzozo wa kinyumbani. Kwa vyovyote vilekatika kutokubaliana, hatupaswi kamwe kutumia vurugu. Ukatili wa kijinsia hauna nafasi katika jamii yetu.” Alisema gavana Anne Waiguru.
Mshukiwa ambaye ni mhubiri katika kanisa moja jijini Nakuru, anadaiwa kutekeleza kisa ambapo alimvamia mkewe kwa silaha yenye makali na kumwacha na majeraha makali kabla ya kutoroka.
Inaarifiwa kuwa mshukiwa alijaribu kuwavamia wanawe wawili wenye umri wa miaka miwili na kumi kabla ya majirani kuingilia kati na kuwaokoa.
Akidhibitisha kisa hicho, afisa mkuu wa jinsia katika kaunti ya Nakuru Gladys Kamuren, aliwataka wakaazi kuwa na utulivu uchunguzi unapoendelezwa na polisi wa kumkamata mshukiwa.
Mwathiriwa anaendelea kupata matibabu katika hospitali moja kwenye kaunti hiyo chini ya uangalizi mkali kutokana na hofu ya wanafamilia wake kuhofia kuwa anaweza kushambuliwa tena.
Ukatili wa mhubiri huyo kwa mke wake unajiri saa chache baada ya rais William Ruto kukashifu visa vya wanawake kuuliwa nchini huku akitenga shilingi milioni mia moja kuendesha kampeni ya kuhamasisha wananchi dhidi ya ukatili kwa wanawake.
Katika miezi michache
ya hapo nyuma, idadi ya mauaji dhidi ya wanawake iliripotiwa kukithiri, data za
utafiti zikionyesha kuwa angalau wanawake 97 waliuliwa ndani ya miezi mitatu
pekee.