Kisa cha kusikitisha kiliripotiwa katika eneo la Juja, Kaunti ya Kiambu ambapo mwanamume mmoja aliyetambulika kwa jina la Alex Kalului anadaiwa kuuawa kwenye mapigano kati ya makundi mawili.
Kalului alikuwa mtunza bustani katika boma moja eneo hilo na alikuwa akijivinjari na marafiki zake katika eneo la Mwireri wakati mapigano yalipozuka siku ya Jumatano usiku.
Polisi walisema mabishano na vita vilichochewa na Ligi Kuu ya Uingereza. Mabishano yaligeuka kuwa vita mbaya na Kalului akaachwa bila fahamu.
Alipelekwa katika Hospitali ya Thika Level Five ambako alifariki alipokuwa akipatiwa matibabu.
Mwili wa marehemu ulihamishiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha General Kago Hospital ukisubiri uchunguzi wa maiti.
Haya yanajiri baada ya shabiki mmoja wa Man United kutoka Uganda kufariki baada ya kushambuliwa na shabiki wa Arsenal kwa kusherehekea bao la Liverpool.
Mwishoni mwa mwezi jana, iliripotiwa kwamba maafisa wa usalama katika eneo la Kabale, Magharibi mwa Uganda walikuwa wanamsaka shabiki mmoja wa Arsenal aliyedaiwa kumshambulia shabiki wa Manchester United.
Tukio hilo lilitokea kufuatia sare ya 2-2 ya Arsenal na Liverpool katika mechi yao ya mkondo wa kwanza iliyochezwa kwenye Uwanja wa Emirates.
Kwa mujibu wa gazeti la Daily Monitor, tukio hilo lilitokea katika Kituo cha Biashara cha Kyobugombe katika Kata ndogo ya Kaharo, Wilaya ya Kabale.
Ilisemekana kuwa marehemu Benjamin Okello alipoteza maisha baada ya mabishano makali na mshukiwa aliyetambulika kwa jina la Onan wakati wa kutazamwa kwa mechi na baada ya filimbi ya mwisho.
Walioshuhudia wanadai kuwa malumbano yalizuka kufuatia bao la kusawazisha la Liverpool katika dakika ya 81.
Shabiki wa Man United, Okello, alishindwa kuzuia furaha yake baadaya kushuhudia bao la kusawazisha la Liverpool na akaanza kusherehekea kwa furaha, jambo ambalo liliripotiwa kumkera Onan ambaye nio mfuasi sugu wa Arsenal. Mabishano yalizuka, yakazidi kwa haraka.
Kwa hasira, Okello alimrushia Onan popcorns alizokuwa ameshika, jambo ambalo lilisababisha makabiliano makali.
Baada ya mechi kumalizika, hali ilizidi kuwa mbaya na kugeuka kuwa ya vurugu. Hapo ndipo Onan anadaiwa kuokota fimbo na kumpiga Okello, na kumuacha akiwa amejeruhiwa vibaya.
Kamanda wa Polisi wa Wilaya hiyo Bw. Joseph Bakaleke, alisema mamlaka bado inaendelea kumsaka mshukiwa Onan ambaye amejificha kufuatia tukio hilo.
Mwenyekiti wa kata ndogo ya Kaharo LCIII Bw. Edmond Tumwesigye alifichua kuwa mshukiwa anaaminika kuwa na umri wa miaka 30 na ni mkazi wa mtaa mmoja na marehemu.