Wakfu wa SMACHS, shirika lisilo la kifaida linaloendeshwa na vijana, limezindua mabalozi vijana 82 kwa madhumuni ya kuendeleza juhudi za kutokomeza njaa na mabadiliko ya hali ya hewa katika kaunti 46 kote nchini.
Mabalozi
hao wa umri wa miaka kati ya 18 hadi 32, wametikwa jukumu la kupigania kilimo cha
kisasa kinachozingatia hali ya hewa na kuhamasisha vijana wenzao kukumbatia
kilimo na kuzuia mabadiliko ya hali ya hewa chini ya mkakati kabambe wa
mwanzilishi unaoitwa "The 30 Things".
Mwanzilishi na mlezi wa wakfu huo Charlene Ruto, akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mabalozi hao iliyofanyika katika taasisi ya elimu maalum ya Kenya (KISE) jijini Nairobi alisisitiza haja ya vijana kukabiliana na changamoto za kisasa akisema kuwa sio tu wahanga wa mabadiliko ya tabia nchi bali ni wabunifu na mawakala wa mabadiliko.
“Vijana sio tu wahasiriwa wa mabadiliko ya hali ya hewa na uhaba wa chakula. Kupitia ubunifu wao, uongozi, na ujuzi, wana uwezo wa kubadilisha uzalishaji wa chakula na kuendesha hatua za hali ya hewa kwa mustakabali endelevu.” Alisema Charlene Ruto.
Katika mchakato wa kuwateua mabalazo hao, vijana 1,600 walivutiwa na kutuma maombi ya kuchaguliwa ila ni vijana 82 pekee waliobahatika kupata fursa hiyo. Vigezo vilivyotumika kuchagua mabalozi hao ni uwezo wao wa uongozi, shauku yao kwa kilimo na hali ya hewa, uwezo wa kutatua matatizo na fikra za ubunifu. Hata hivyo, mpango huo ulilenga kuajiri mabalozi 94 angalau mabalozi 10 kwa kila kaunti. Baadhi ya kaunti zilikuwa na waombaji wachache, huku kaunti ya Lamu ikikosa kabisa waombaji.
Nchini Kenya, kwa mujibu wa data za serikali, sekta ya kilimo licha ya kuwa muhimu kwa uchumi wa Kenya, ushiriki wa vijana katika kilimo unasalia chini ya asilimia 30. Wakfu wa SMACHS, hata hivyo unalenga kuimarisha kilimo kuwa cha kisasa kupitia suluhu za kidijitali na mitambo, kwa kuwa sekta hiyo ina uwezo wa kufungua fursa kubwa za ajira kwa vijana 800,000 wanaoingia kazini kila mwaka.
Mradi huo wa SMACHS unaendana na matokeo ya ripoti ya 2023 ya Mahitaji ya Vijana wa Kiafrika ya hatua ya hali ya hewa ya UNFCCC, ambayo ilifichua kuwa vijana wa Kiafrika wana wasiwasi mkubwa juu ya mabadiliko ya hali ya hewa na wana hamu ya kushirikiana na serikali na mashirika kuunda suluhisho ya kibunifu.
Wakfu wa SMACHS unawezesha kizazi kipya cha viongozi kuunda
upya mandhari ya kilimo ya Kenya, kuendesha usalama wa chakula, kustahimili
hali ya hewa, na ukuaji wa uchumi kwa taifa kupitia kilimo cha kimitambo.