Rais William Ruto amewahimiza vijana wa Kenya kuwa wazalendo na wasikubali mtu kulidharau taifa lao.
Akizungumza katika eneo la Manyani kaunti ya Taita Taveta katika hafla ya kufuzu kwa maafisa wa huduma ya wanyamapori katika chuo cha kutekeleza sheria cha huduma ya wanyamapori nchini, Ruto alisema kuwa Kenya ni nyumbani kwa wote na ni jukumu la kila mmoja kuilinda kwa ushirikiano .
Ruto aliwahimiza vijana kuwa wazalendo kila wakati na kuliweka taifa mbele akieleza kuwa ni jukumu la vijana kulinda nchi na kutoruhusu wachache wenye nia mbaya kuharibu jina la taifa.
‘’Lazima tujue kwanza kama Wakenya wazalendo kuwa lazima tusimame, tuitetee na tuilinde nchi yetu. Tusikubali watu wenye nia hasi kuharibu, kudhalilisha na kusambaza ujumbe mbaya kuhusu nchi yetu. Kenya ni kwetu na lazima tuilinde pamoja nawaomba vijana wetu kuelewa kuwa huwezi dhalalisha nchi yako ya mama. Lazima tuinuke na tuitetee Kenya,’’ Alisema Ruto.
Kiongozi huyo wa taifa aliongeza kuwa anafurahia nchi ya Kenya kuwa na vijana ambao wako radhi kusimama na kuilinda nchi yao kwa liwe liwalo. Aliwahimiza wazazi wa maafisa waliofuzu kuwapatia usaidizi wanaohitaji ili kufauli katika jukumu lao kama maafisa kwenye idara ya wanyamapori nchini.
Rais alisistiza kuwa serikali ya Kenya Kwanza anayoongoza itaunga mkono maafisa hao katika juhudi zao ya kulinda urithi wa taifa.
‘’Nimefurahi sana kwamba tuko na wananchi wazalendo. Wanaume na wanawake ambao wamepata mafunzo na wako tayari wakiwa na nguvu nyingi na kwa uzalendo kuilinda nchi yetu na kuhifadhi pori zetu. Nitawaunga mkono pamoja na serikali yangu ili kuhakikisha kuwa mnatimiza wajibu wenyu na kuhakikisha kuwa mnapata raslimali na vifaa ili mtekeleze wajibu wenyu na mtumikie nchi tunayoipenda sote; nchi yetu ya Kenya." Alisema Rais.