Seneta wa kaunti ya Nairobi Edwin Sifuna amependekeza kuimarishwa kwa uhusiano wa kibiashara kati ya Kenya na taifa la Somalia ili taifa hilo liagize miraa kwa wingi.
Sifuna amesema hayokatika kikao cha bunge la seneti mnamo Jumanne akielezea kuhusu safari yake nchini Somalia.
Kwa mujibu wa seneta huyo, katika ziara yake nchini Somalia alipata fursa ya kuonja miraa inayokuzwa nchini Ethiopia na kugundua kwamba miraa inayokuzwa nchini Kenya ni bora ikilinganishwa na ile ya kutoka Ethiopia.
“Uhusiano wetu wa kibiashara na Somalia lazima uimarishwe kwa sababu tunapozungumza sasa hivi wanaagiza Miraa kutoka Ethiopia na nilipata fursa ya kuonja miraa hiyo na kugundua kwamba miraa yetu ni bora zaidi.” Alisema Edwin Sifuna.
Katika pendekezo la seneta Sifuna, ametaka seneta wa Meru kujumuishwa katika orodha ya wabunge na maseneta watakaosafiri kuelekea nchini Somalia kwa ajili ya kuapishwa kwa raia mpya wa nchi hiyo. Sifuna amesema hayo akirejelea barua kutoka kwa wajumbe wa Somaliland ambayo amesema kwamba anafahamu imetumwa kwa maseneta wa mabunge mawili ya Kenya ikiwaalika baadhi ya viongozi kuhudhuria uapisho wa rais mpya wa taifa hilo.
Seneta huyo amesema kwamba ikiwa atahusishwa kwenda kuhudhuria hafla hiyo ya uapisho, nafasi yake atampa seneta Murungi Kathuri wa Meru ambaye pia ni naibu spika wa seneti ili kuwasilisha hoja ya diplomasia ya biashara kama naibu spika wa seneti.
“Ningependa orodha hiyo iwe na seneta wa Meru. Hata kama sitaki kwenda
bwana spika, nitapeana nafasi yangu kwa sababu ajenda hii ya kidplomasia ya biashara
ni vizuri ikisukumwa na naibu spika huyo pamoja na mwanachama wa Njuri Ncheke.” Alisema Edwin Sifuna.