Gavana wa kaunti ya Trans Nzoia George Natembeya amewataka wananchi wa kaunti hiyo kuwawajibisha wawakilishi wa wadi katika kaunti hiyo ili kuhakikisha miradi ya maendeleo na pesa za umma zinatumika kwa njia inayostahili.
Akizungumza katika hafla ya kuadhimisha sherehe za Jamhuri katika kaunti hiyo, gavana Natembeya amesema kwamba fedha zinatolewa na serikali ya kaunti kwa wawakilishi wadi kwa minajili ya kuendeleza miradi na maendeleo.
Gavana huyo amesema kwamba wakati wadi nyingine zina miradi ya maendeleo ikiwemo zahanati, barabara nzuri, madarasa ya chekechea, maji na wakulima wako sawa, ni kutokana na fedha ambazo serikali yake inasambaza na kutumiwa vizuri na wawakilishi wa wadi.
Kutokana na hilo, Natembeya amewashauri wananchi kuzuru katika ofisi za wadi ili kupata taarifa ya maendeleo yaliyofanywa na wawakilishi wao wa wadi akifichua kwamba serikali yake tangu aingie mamlakani, imetoa jumla ya shilingi takribani milioni mia moja kwa wadi za kaunti hiyo.
“Ukiona wadi moja iko na barabara, madarasa ya ECDE, zahanati, maji na wakulima wako sawa sawa na ingine haina enda angalia uongozi wa ile wadiunakaa namna gani.” Alisema Natembeya.
Natembeya amewataka wananchi kufanya vikao na wawakilishi wadi ili kupanga miradi katika wadi zao.
Vile vile gavana huyo aliyekuwa mratibu wa bonde la ufa kabla ya kuingia katika siasa aliwaonya wawakilishi wa wadi kwamba barabara zote lazima zitengenezwe vizuri kutumia shilingi milioni mia nne zilizosambazwa kwenye wadi zote katika kaunti hiyo.
“Tumekubaliana
na MCA kwamba barabara wakati huu zitengenezwe vizuri, hatutaki kulima tu
barabara na greda mvua ikinyesha inakuwa ni matope kila mahali. Tunataka
barabara itengenezwe vizuri hata wakati mvua inanyesha kusikuwe na matope kwa
barabara.” Alisema gavana George Natembeya.
Katika
kufanikisha haya, Natembeya aliwataka wananchi kuwajibika na kuhusika katika
maswala ya uongozi na wawakilishi wao wa wadi kama ilivyo katika katiba ya
Kenya.