Kithure Kindiki amewaonya wanasiasa haswa kutoka kwa mrengo wa aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua dhidi ya kuvuruga na kuchochea utendakazi wa serikali ya rais William Ruto ikiwemo kuvuruga baadhi ya mikutano ya kisiasa ya Kenya kwanza.
Naibu wa rais alisema hayo katika hafla ya maombi iliyofanyika kwenye kanisa la Full Gospel katika eneo la Kamumu kaunti ya Embu mnamo Jumapili 5, Januari 2025.
Naibu kiongozi huyo wa chama cha UDA, ambaye alionekana mwenye hasira aliwaonya wanasiasa wanaopinga serikali dhidi ya uchochezi na kuvuruga amani haswa katika hafla za mikutano ya wanasiasa kutoka upande wa serikali.
Licha ya kutotaja majina halisi ya wanasiasa hao Kindiki alisema kuwa naibu rais wa zamani Rigathi Gachagua hatopewa ruhusa ya kuendeleza siasa za kutawanya watu na kuvuruga amani ya nchi.
Katika hotuba yake, aliwaonya wanasiasa dhidi ya kueneza sera za uwongo dhidi ya serikali na kukosa heshima dhidi ya wanasiasa wenzao, akiongeza kuwa serikali haitaruhusu mtu yeyote ambaye anajaribu kupanda mbegu ya chuki miongoni mwa Wakenya bila kutoa suluhu ya kudumu ya kutatua changamoto zinazowakumba Wakenya.
‘’Uongozi sio kujipiga kifua bali ni kutoa suluhisho, mungu amekubariki na nafasi ya kuhudumia watu na unaanza kutukana viongozi wengine ni jambo mbaya sana. Hatutaruhusu mtu yeyote kuzunguka akichochea wakenya na kutoa malalamishi bila kuleta suluhu,’’ Alisema naibu rais.
Onyo la naibu wa rais linajiri siku chache baada ya sehemu ya Wakenya kulalamika kuwa hakuwatakia kheri wakati wa msimu wa krisimasi na maka mpya. Vile vile, kiongozi huyo katika siku za hivi karibuni alikosa kuonekana hadharani haswa katika sherehe za kitamaduni za jamii ya Dholuo, kwenye ikulu ndogo ya rais njini Kisii alikokuwa rais na kwenye mashindano ya soka yaliyoandaliwa na gavana Gladys Wanga kaunti ya Homa Bay.
Kindiki hata hivyo alijitetea katika hafla ya harusi ya mwana wa waziri wa utalii Rebecca Miano, alipokiri kuwa alipewa rukhsa ya muda wa kupumzika na rais William Ruto.
Kindiki aliwahimiza viongozi wote nchini kujiepusha na tabia
ya kuvuruga mkutano za kisiasa ambazo zinafanywa na wapinzani wao. Aliongeza
kuwa mlima kenya ni eneo moja na kuwarai wananchi kukataa kugawanjwa
kwa msingi wowote.