Aliyekuwa
naibu wa rais Rigathi Gachagua amemuandikia ujumbe maalum gavana wa Trans Nzoia
George Natembeya akimuonyesha sapoti huku kukiwa na mjadala mkubwa nchini
kuhusu mzozo wake wa hivi majuzi na baadhi ya viongozi wengine wakati wa
mazishi katika kaunti ya Bungoma.
Siku ya Ijumaa, wakati wa mazishi ya mamake spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula na Mbunge wa Westlands Tim Wanyonyi, gavana Natembeya alitofautiana hadharani na bosi wa COTU Francis Atwoli na kiongozi wa wengi katika Bunge Kimani Ichungw'a kuhusu suala la visa vya hivi majuzi vya utekaji nyara.
Matukio yaliyojiri wakati wa maziko hayo yalipokewa kwa hisia mseto huku baadhi ya wananchi na viongozi wakimkosoa bosi huyo wa Trans Nzoia wakati wengine wakiunga mkono kauli alizotoa.
Kwenye ujumbe wake kwa Natembeya Jumapili jioni, Gachagua alimtaka mkuu huyo wa kaunti kutotikiswa na kuendelea na kazi yake bila kusumbuliwa.
“Ndugu yangu Mpendwa Gavana Natembeya. Tafadhali usiwaruhusu Washairi wa Mahakama na Wastadi wa matamshi kukusumbua kutoka kwa kazi unayofanya ya kuwasilisha kwa watu wa Kaunti ya Trans-Nzoia. Wakosoaji hawa wa Mahakama wako kwenye kazi potofu ya kutoa ahueni ya katuni kwa bwana wao," Gachagua aliandika kwenye Twitter.
"Na usiogope kusema kwa niaba ya watu wa Kenya inapobidi. Kejeli na ukosoe unazotupiwa ni ushuhuda wa wazi kwamba unaleta athari unapozungumza ukweli kwa mamlaka," aliongeza.
Gachagua alimtaka gavana huyo wa awamu ya kwanza kuendelea kuwaunganisha watu na kuweka maslahi ya wananchi mbele.
"Ombi langu ni kwamba muendelee kufanya hivyo, na muwaunganishe watu wenu na kulinda utu na fahari yao ya kisiasa. Umoja huu, ninawahakikishia, utahakikisha kwamba maslahi ya watu wenu daima yanakuwa mbele na katikati ya mwelekeo wa utawala wowote. Mungu aendelee kuwa nawe,” aliongeza.
Majibizano makali yalishuhudiwa wakati wa mazishi ya marehemu Mama Anne Nanyama, mamake Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula siku ya Ijumaa, huku viongozi wakizozana kuhusu visa vya utekaji nyara vilivyoongezeka.
Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah alishindwa kujizuia na kumkemea gavana wa Trans Nzoia George Natembeya kuhusiana na matamshi yake kuhusu utekaji nyara na mauaji ya watu nje ya mahakama.
Shambulio hilo lilijiri baada ya Natembeya kutokubaliana na matamshi ya Boss wa Cotu Francis Atwoli kuhusu utekaji nyara.