Rais
William Ruto ameomboleza kifo cha nduguye Gavana wa Meru Kawira Mwangaza Eric
Kimathi, ambaye alijulikana kama Steroo.
Katika taarifa, Ruto alimtaja Steroo kama kijana mjasiriamali aliyebadilisha maisha ya watu wengi.
Ruto aliendelea kusema kuwa Steroo alikuwa mtu mkarimu na mchapakazi ambaye alikuwa na mawazo mengi mazuri.
Rais aliomba faraja ya Mungu huku familia ikiendeliea kukubali kifo chake.
"Tunasherehekea maisha ya mtu mjasiriamali na mwenye mawazo mazuri ambayo yalibadilisha maisha ya watu wengi. Eric Kimathi ‘Steroo’ — kaka yake Gavana Kawira Mwangaza — alikuwa mkarimu, mchapakazi na mwenye maendeleo. Mawazo yetu yako pamoja na familia katika wakati huu mgumu. Pumzika kwa Amani, Steroo,” Ruto alisema.
Matamshi yake yamejiri saa chache baada yake pia kufariji familia ya Naibu Gavana wa Meru Isaac M'Ethingia kufuatia kifo cha mamake.
Katika salamu zake za faraja, Rais alimueleza Mama Joyce kuwa ni mcha Mungu na ameitakia familia yake faraja ya Mungu wakati wakiomboleza kifo chake.
"Rambirambi zetu kwa Naibu Gavana wa Meru Isaac M'Ethingia kwa kuondokewa na mamake mpendwa, Joyce. Alikuwa mwanamke mwajibikaji, mcha Mungu na mwenye maendeleo ambaye alijitolea kutumikia jamii," Ruto alisema.
"Mungu aifariji familia na watu wa Meru katika kipindi hiki cha majonzi. Pumzika kwa Amani."
Steroo
alifariki Ijumaa wiki iliyopita.
Kifo chake kilitangazwa na dadake Mwangaza kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.
Mazishi yamepangwa kufanyika Jumamosi, Januari 18, 2025.
“Nimehuzunika sana kutangaza kifo cha kaka yangu mpendwa Erick Kimathi (Stero) leo Asubuhi 10 Januari 2025 baada ya kuugua kwa muda mrefu. Kwa hivyo ulipigana kwa ushujaa. Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Mazishi ya Jumamosi tarehe 18 Januari 2025 katika Kijiji cha Mathagiro Timau Buuri,” Gavana Mwangaza aliandika kwenye Facebook.