Askari
wa magereza ambaye alijiunga waziwazi na Wakenya katika maandamano ya kupinga muswada
wa fedha mnamo Juni alishtakiwa Jumatatu kwa kuchapisha habari za uwongo
zinazogusa wimbi la hivi majuzi la utekaji nyara.
Kulingana na karatasi ya Mashtaka, Jackson Kuria Kihara almaarufu Cop Shakur, mnamo Januari 11, 2025, kwa pamoja na wengine ambao hawakuwa mbele ya mahakama, walichapisha habari za uwongo kwa kujua na kinyume cha sheria, wakitumia Akaunti ya X Corp @CopShakur.
Shakur alikaa wikendi nzima chini ya ulinzi wa polisi huku maafisa wakitaka kumshikilia kwa uchunguzi zaidi.
Mshtakiwa alifikishwa katika mahakama ya Milimani ambapo alionekana akiwa amevalia t-shati yenye picha ya marehemu mfanyibiashara Jacob Juma upande wa mbele.
Alikamatwa mnamo Januari 15, katika makazi ya wafanyikazi wa gereza la Kamiti Maximum na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Muthaiga kabla ya kufikishwa kortini chini ya maombi tofauti.
DCI waliambia mahakama kuwa wakati wa kukamatwa kwake, simu yake ilinaswa na wanahitaji muda wa kutosha kuifanyia uchunguzi wa kimahakama.
"Kwa sababu ya wingi wa data inayotarajiwa na ushahidi wa kidijitali unaohusika ambao bado haujachunguzwa na kuchambuliwa kwa kina, kuna haja ya kuongezwa kwa muda ili kuwezesha uchunguzi unaoendelea," ilisoma karatasi ya DCI kwa sehemu.
Pia walisema kuwa Shakur, akiwa afisa wa huduma aliyefunzwa, ana uwezo wa kuingilia uchunguzi kwa vile amefunzwa matumizi ya silaha.
DCI ilikuwa imemwambia Hakimu Mkuu Lucas Onyina kwamba walihitaji siku 21 zaidi ili kuwawezesha kukamilisha uchunguzi.
Lakini mahakama iliwapa siku tatu kukamilisha uchunguzi wao.
Wakati huo walikuwa wakimchunguza kuhusu uhalifu wa mtandaoni na makosa ya uasi.
Jumatatu aliachiliwa kwa dhamana ya pesa taslimu Sh50,000 baada ya kukana mashtaka mbele ya Hakimu wa Milimani Gilbert Shikwe.