Mwili wa Raymond ulipatikana Jumapili asubuhi, 19 Januari 2025, karibu na lango la nyumba yake ya kukodi baada ya kuuawa na washambuliaji wasiojulikana Jumamosi jioni.
Katika taarifa yake Jumatatu asubuhi, Gachagua alidai kuwa kitendo hicho ni njia ya kuzua hofu kwa wakosoaji wa serikali na akakikemea vikali.
“Kiwango cha kutovumiliana kisiasa na ukandamizaji katika nchi yetu kinafikia viwango visivyo na uwiano na vya kutisha. Mauaji ya kutisha na ya kikatili ya Raymond Otieno wa Molo wikendi ni shuhuda tosha wa mkakati mwingine wa kuzua hofu miongoni mwa Wakenya katika mkakati wa kusikitisha na wa kizamani wa kuwanyamazisha wakosoaji wa serikali baada ya utekaji nyara kukosa kufanya kazi. Je, taifa kubwa kama Kenya linawezaje kutumbukia katika handaki za Nchi iliyoshindwa ambapo watoto na wanawake hawana nafasi ya kupumua?” Gachagua alisema.
Naibu rais huyo wa zamani aliifariji familia ya marehemu mwanaharakati huyo na kumuomboleza kama mtetezi mkuu wa haki za binadamu.
Pia ametaka hatua za haraka zichukuliwe dhidi ya wauaji wa kijana huyo.
“Tunapoomboleza kifo cha kijana huyu, ambaye alikuwa mtetezi na bingwa wa haki za binadamu, tunaomba haki itendeke. Wauaji wake lazima waadhibiwe kwa vyovyote vile. Serikali ya Kenya haiwezi kumudu kuketi kwenye uzio kuhusu suala hili,” alisema.
"Mungu ailaze Roho ya Raymond Otieno mahali pema peponi na afariji familia yake na watu wa Molo," aliongeza.
Otieno aliuawa kinyama Jumamosi usiku mwendo wa saa tano usiku alipokuwa akielekea nyumbani.
Washirika wa karibu wanadai kuwa aliripotiwa kupokea vitisho vya kuuawa kutoka kwa watu wasiojulikana katika siku zilizopita.
Polisi walisema wanachunguza mauaji hayo.
Mbunge wa Molo Kuria Kimani aliomboleza kifo hicho siku ya Jumapili na kuwataka polisi kupata undani wa kisa hicho.