Waziri
wa Utumishi wa Umma Justin Muturi alikosa kuhudhuria mkutano wa kwanza wa
Baraza la Mawaziri wa 2025 uliofanyika katika Ikulu ndogo ya Kakamega mnamo
Jumanne.
Mkutano huo ulioongozwa na Rais William Ruto ulifikia maazimio kadhaa, ikiwa ni pamoja na kuunganishwa kwa mashirika 42 ya serikali kuwa mashirika 20 kama hatua ya kupunguza gharama.
Picha za mkutano huo zilizofikia Radio Jambo zilionyesha kuwa mawaziri wote wa baraza la mawaziri la Ruto isipokuwa Muturi walikuwepo.
Kutokuwepo kwa Mwanasheria Mkuu huyo wa zamani katika mkutano huo muhimu kumeibua sintofahamu na mjadala mkubwa huku wengi wakishuku kuwa kunahusiana na mzozo wake wa hivi majuzi na Serikali kuhusu sakata la utekaji nyara wa wakosoaji wa serikali.
Wakati wa kikao na wanahabari katika hoteli ya Serena mapema mwezi huu, Muturi alisema familia yake ilipitia mateso na misukosuko baada ya mwanawe kutekwa nyara na kutoweka bila habari yoyote kutoka kwa polisi.
Waziri alisema hii ilikuwa licha ya kutoa maombi na matakwa kadhaa kwa ngazi zote za vyombo vya usalama kusaidia kumtafuta.
"Sikuwa na uhakika kama alikuwa hai au amekufa, jambo lililotufanya tuhangaike na kuniacha mimi, mke wangu na familia yangu katika msukosuko," alisema.
Muturi alisema zaidi ya miezi sita baada ya masaibu hayo na kuachiliwa kwake na watekaji nyara, hakuna aliyefunguliwa mashtaka na hakuna aliyeeleza ni kwa nini mwanawe alitekwa nyara na kuzuiliwa.
Waziri huyo wa Utumishi wa Umma alitoa wito wa majadiliano ya wazi juu ya utekaji nyara unaoendelea akishutumu hali ya kuhusika katika katika kitendo hicho.
Alisema serikali haiwezi kudhani kuwa haina hatia katika suala hilo ambalo alisisitiza kuwa kuna hatari ya kuiingiza nchi katika machafuko.
Muturi alisema jinsi utekaji nyara huo unavyotekelezwa mchana kweupe unathibitisha kuwa una baraka zote za serikali.
“Mimi nafahamu kabisa fundisho la uwajibikaji wa pamoja, lakini kwa kuwa mimi pia ni mhanga wa kutekwa na kutumikia serikali hii sijapata majibu, nimechukua hatua hii isiyo ya kawaida ili suala hilo lijadiliwe kwa uaminifu na ukweli. kwa uwazi kama nchi kwa nia ya kutafuta suluhu la kudumu."