logo

NOW ON AIR

Listen in Live

DCI wakiri kumkamata mgonjwa aliyeshiriki maandamano katika afisi za Wizara ya Afya, waeleza sababu

Bi Mulei alipelekwa katika Kituo cha Polisi cha Upper Hill, ambapo anazuiliwa akisubiri kupelekwa mahakamani.

image
na Samuel Mainajournalist

Yanayojiri24 January 2025 - 08:02

Muhtasari


  • DCI walisema kuwa mshukiwa alifuatiliwa hadi katika Barabara ya Hombe, nje ya Barabara ya Juja, na akakamatwa.
  • Wakenya kwenye mitandao ya kijamii, mashirika ya kiraia, na wadau wengine wamedai kuachiliwa kwake na kufutwa kwa mashtaka dhidi yake.


Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) mnamo Alhamisi ilimkamata mshukiwa Grace Njoki Mulei kwa madai ya kusababisha fujo katika chumba cha Bodi ya Wizara ya Afya wiki jana.

Katika taarifa Alhamisi jioni, DCI walisema kuwa mshukiwa alifuatiliwa hadi katika Barabara ya Hombe, nje ya Barabara ya Juja, na akakamatwa.

"Amepelekwa katika Kituo cha Polisi cha Upper Hill, ambapo ataendelea kuzuiliwa hadi kesi yake itakapopangwa kufanyika kesho (Ijumaa)," DCI ilisema.

Mulei ambaye ana umri wa miaka 61, alikuwa mmoja wa wagonjwa waliotembelea ofisi za Wizara ya Afya mnamo Januari 15, 2025, kupinga ukosefu wa usawa wa bima ya SHA na ukosefu wa ufanisi.

Wakenya kwenye mitandao ya kijamii, mashirika ya kiraia, na wadau wengine wamedai kuachiliwa kwake na kufutwa kwa mashtaka dhidi yake.

Chama cha Madaktari wa Kenya, Chama cha Wanasheria wa Kenya, na Kikundi Kazi cha Marekebisho cha Polisi wameelezea wasiwasi kwamba wagonjwa wengine waliokuwa na Mulei wako katika hatari ya kukamatwa pia.

Walisisitiza kuwa kutetea kuboreshwa kwa huduma za afya ya umma si kosa bali ni wajibu wa kiraia kuhakikisha huduma za afya zinazookoa maisha kwa jamii yenye afya na usawa zaidi.

"Tunatoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka kushughulikia ukiukwaji huu, kulinda haki za wagonjwa, na kuendeleza mazingira ambapo huduma za afya zinaweza kupatikana kwa uhuru na bila hofu," walisema katika taarifa.

Walisema vitendo hivyo ni ukiukaji wa haki za kimsingi za wagonjwa na kikwazo kikubwa cha kupata huduma muhimu za afya.

"Kila mtu, bila kujali utetezi au maoni yake, anastahili haki ya afya bila hofu ya vitisho, kunyanyaswa, au kukamatwa," taarifa hiyo iliongeza.

Ripoti ziliibuka siku ya Alhamisi jioni kwamba Bi Mulei alidaiwa kutekwa nyara na kupelekwa kusikojulikana.

Hili lilizua hasira nyingi kwenye mitandao ya kijamii huku Wakenya wakilaani kitendo hicho kabla ya polisi kuthibitisha kumkamata.



RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved