Kifo cha Aga Khan kilitangazwa na shirika lake la hisani la Aga Khan Development Network Jumatano asubuhi. Aliaga dunia kwa amani mjini Lisbon mnamo tarehe 4 Februari 2025 akiwa na umri wa miaka 88.
Huku akimuomboleza Jumatano asubuhi, Rais Ruto alimtambua marehemu kuwa kiongozi wa kipekee aliyejitolea kuwasaidia watu wasiojiweza.
"Tumehuzunishwa na kifo cha The Aga Khan, kiongozi wa kiroho wa Waislamu wa Ismailia," Ruto alisema katika taarifa kwenye akaunti yake ya X.
"Alikuwa kiongozi wa ajabu ambaye alienda zaidi ya kile kilichoonekana kuwa ngumu kusaidia walio hatarini - kupitia misaada yake katika hospitali na shule," taarifa hiyo ilisoma zaidi.
Amiri Jeshi Mkuu aliendelea kuwapa pole familia ya Aga Khan na Waislamu wote wa Ismailia huku akiitaka roho ya marehemu ipumzike kwa amani.
Prince Karim Aga Khan alikuwa imamu wa 49 wa urithi wa Waislamu wa Ismailia, ambaye anafuatilia nasaba yake moja kwa moja hadi kwa Mtume Muhammad.
Shirika lake la hisani, Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan, lilitangaza kifo chake siku ya Jumanne katika taarifa.
"Mtukufu Prince Karim Al-Hussaini, Aga Khan IV, Imam wa 49 wa kurithi wa Waislamu wa Shia Ismailia na kizazi cha moja kwa moja cha Mtume Muhammad (rehema na amani ziwe juu yake), alifariki dunia kwa amani jijini Lisbon tarehe 4 Februari 2025, mwenye umri wa miaka 88, akiwa amezungukwa na familia yake," taarifa hiyo inasomeka kwa sehemu.
Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan ulisema mrithi wake atatangazwa hivi karibuni.
“Tangazo la mrithi wake mteule litafuata.Viongozi na wafanyakazi wa Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan tunatoa pole kwa familia ya Mtukufu na kwa jumuiya ya Ismailia duniani kote. Tunapoheshimu urithi wa mwanzilishi wetu, Prince Karim Aga Khan, tunaendelea kufanya kazi na washirika wetu kuboresha hali ya maisha ya watu binafsi na jamii kote ulimwenguni, kama alivyotaka, bila kujali itikadi zao za kidini au asili,” taarifa ilisomeka zaidi.
Aga Khan alimrithi babu yake, Sir Sultan Mahomed Shah Aga Khan III, kama Imamu wa Waislamu wa Shia Ismailia mwaka 1957 akiwa na umri wa miaka 20.
Tangu wakati huo, amejitolea juhudi zake za kuboresha hali ya maisha ya watu walio hatarini zaidi, akisisitiza mtazamo wa Uislamu kama imani inayofundisha huruma na uvumilivu na inayoshikilia utu wa mwanadamu.