Baada ya kifo cha Kiongozi wa Kiroho wa Waislamu wa Ismailia, Aga Khan IV, mwanawe mkubwa, Prince Rahim Al-Hussaini, ametangazwa kuwa mrithi wake, akichukua nafasi kama Aga Khan V.
Aga Khan IV, ambaye aliongoza kwa zaidi ya miaka 67, alifariki Februari 4, 2025 akiwa na umri wa miaka 88. Uongozi wake ulijikita katika maendeleo ya kijamii, elimu, afya, na uhifadhi wa tamaduni, akihamasisha maendeleo kupitia Shirika la Aga Khan Development Network. (AKDN)
Prince Rahim, ambaye kwa muda mrefu amekuwa akihusika katika shughuli za maendeleo chini ya AKDN, sasa anaingia rasmi katika nafasi ya juu ya uongozi wa kiroho na kijamii wa jumuiya ya Ismailia, ambayo ina wafuasi kati ya milioni 12 hadi 15 duniani kote.
Tangu ujana wake, amekuwa akifanya kazi bega kwa bega na baba yake, hasa katika masuala ya kulinda mazingira na kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Aga Khan IV, ambaye jina lake halisi lilikuwa Shah Karim Al-Hussaini, alichukua uongozi wa jumuiya hiyo mwaka 1957 akiwa na umri wa miaka 20, baada ya kurithi nafasi hiyo kutoka kwa babu yake.
Katika kipindi chake cha uongozi, alifanya kazi kubwa ya kuimarisha maisha ya wafuasi wake na jamii kwa ujumla kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo.
Aga Khan IV alianzisha taasisi za elimu kama Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU), hospitali za kiwango cha kimataifa, na miradi ya uhifadhi wa tamaduni kupitia Tuzo ya Aga Khan ya Usanifu.
Kupitia AKDN, alifanikiwa kutekeleza miradi katika zaidi ya nchi 30 duniani, akitoa msaada katika sekta za elimu, afya, na maendeleo ya kijamii. Uongozi wake uliwiana na mtazamo wa Kiislamu kuhusu maendeleo endelevu, akihimiza elimu kwa wote, usawa wa kijinsia, na jitihada za kupunguza umaskini.
Baada ya kifo chake, uteuzi wa Prince Rahim kama Aga Khan V umepokelewa kwa matumaini makubwa na wanajumuiya wa Ismailia.
Wengi wanaamini kuwa ataendeleza kazi ya baba yake kwa bidii, huku akileta mwelekeo mpya katika changamoto zinazokumba ulimwengu wa sasa, hususan masuala ya kijamii, maendeleo endelevu, na matumizi ya teknolojia katika kuinua maisha ya watu.
Uongozi wa Aga Khan V unatarajiwa kuzingatia msingi wa
mafanikio ya baba yake, huku akijaribu kujibu mahitaji mapya ya jamii.
Jumuiya ya Ismailia na wadau wa kimataifa sasa wanatazama kwa hamu hatua atakazochukua katika safari yake mpya ya uongozi.