Washukiwa wanaripotiwa kupanga utekaji nyara wa raia wa kigeni waliokuwa wakifanya kazi kwenye mradi wa ujenzi wa mtaro wa maji.
Uchunguzi wa kina ulibaini kuwa mshukiwa huyo alikuwa ameandaa malipo ya KSh 100,000 kwa mshirika wake wa hapa nchini.
Crime scene
Polisi wa kupambana na ugaidi mnamo Jumanne asubuhi
waliwakamata washukiwa wawili wa kundi la Al Shabaab katika kaunti ya Mandera.
Wawili hao wanaripotiwa kuwa walikuwa wakipanga utekaji nyara
wa raia wa kigeni waliokuwa wakifanya kazi kwenye mradi wa ujenzi wa mtaro wa
maji taka katika mji wa Mandera.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Idara ya Upelelezi wa Jinai
(DCI), msako wa kiintelijensia uliongoza maafisa wa usalama kumkamata mshukiwa
mkuu, Isaac Abdi Mohamed, anayejulikana pia kama Kharan Abdi Hassan, mwenye
umri wa miaka 29.
Inadaiwa kuwa alijipenyeza nchini hivi majuzi kutoka El-Ade,
Somalia, na kutengeneza stakabadhi ghushi ili ajitambulishe kama Mkenya.
Uchunguzi wa kina ulibaini kuwa mshukiwa huyo alikuwa ameandaa
malipo ya KSh 100,000 kwa mshirika wake wa hapa nchini, ambaye angehusika
katika utekelezaji wa utekaji nyara huo.
Aidha, iligunduliwa kuwa washukiwa walipanga kuwahamisha
waathiriwa hadi El-Ade kwa gharama ya KSh 300,000, kwa usaidizi wa mshirika
wake wa pili, Noor Yacob Ali, mwenye umri wa miaka 29.
Katika operesheni nyingine iliyofanyika mapema leo, vikosi vya
usalama vya pamoja vilifanikiwa kumnasa Yacob Ali katika eneo la Metameta,
ndani ya Mandera township.
Kwa sasa, washukiwa hao wanazuiliwa na wanaendelea kuhojiwa
kabla ya kufikishwa mahakamani kwa mashitaka ya kuwa wanachama wa kundi la
kigaidi, kosa linaloangukia chini ya Sheria ya Kuzuia Ugaidi (POTA).
Maafisa wa usalama wamewataka wananchi kushirikiana na vyombo
vya usalama kwa kutoa taarifa za kutiliwa shaka ili kuhakikisha usalama
unadumishwa.