logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Safari ya aliyekuwa mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati

Aliyekuwa mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC nchini Kenya Wafula Wanyonyi Chebukati ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 64.

image
na Japheth Nyongesa

Yanayojiri21 February 2025 - 09:22

Muhtasari


  • Chebukati alisomea Shule ya Upili ya Lenana na baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi ambapo alipata shahada ya Sheria.
  • Aliwahi kuwania kiti cha ubunge cha Eneo Bunge la Saboti mnamo 2007 kwa tiketi ya Orange Democratic Movement (ODM).

Aliyekuwa mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na mipaka  IEBC nchini Kenya Wafula Wanyonyi Chebukati ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 64.

Wafula Chebukati alikuwa anatoka kaunti ya Bungoma alikozaliwa Desemba 22, 1961. Chebukati alisomea Shule ya Upili ya Lenana na baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi ambapo alipata shahada ya Sheria.

Pia alipata shahada ya uzamili katika usimamizi wa biashara kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta.

Zaidi ya hayo, yeye pia alikuwa mwanachama wa Chama cha Wanasheria cha Kenya (LSK), Taasisi ya Makatibu waliothibitishwa, na Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ).

Chebukati alifunga pingu za maisha na mkewe Mary Chebukati mnamo 1990. Wanandoa hao walibarikiwa na watoto watatu, msichana na wavulana wawili.

Yeye amekua Mwanasheria wa Kenya . Mwaka 2006 alianzisha kampuni ya sheria kwa jina Cootow and Associates Advocates iliyokuwa na makao yake jijini Nairobi.

Aliwahi kuwania kiti cha ubunge cha Eneo Bunge la Saboti mnamo 2007 kwa tiketi ya Orange Democratic Movement (ODM).

Aidha, Januari 2017, aliteuliwa na Rais wa Kenya wakati huo Uhuru Kenyatta kujiunga na IEBC kama mwenyekiti akichukuwa mikoba kutoka kwa mwenyekiti wa zamani Isaac Hasan.

Wakati wa uongozi wake, alisimamia chaguzi tatu za Kenya: uchaguzi mkuu wa Kenya wa 2017, uchaguzi wa rais wa marudio wa Oktoba 2017 baada ya kubathirishwa na mahakama kuu chini ya aliyekuwa jaji mkuu David Maraga na  vilevile uchaguzi mkuu wa Kenya wa 2022..

Chebukati alitunukiwa "Elder of the order of the Golden Heart (EGH)' - tuzo ya pili ya juu zaidi ya Kenya anayopewa raia - na Rais wa Kenya kwa ujuzi na hekima yake. Kwa hivyo kumbukumbu yake inapaswa kuheshimiwa na kuenziwa hivyo kuwekwa katika historia ya Kenya.

Mnamo tarehe 17 Februari 2025, bosi huyo wa zamani wa IEBC alilazwa katika hospitali moja jijini Nairobi ambako amekuwa akipatiwa matibabu kwa karibu wiki moja. Vyanzo vya hospitali vilikuwa vimesema kwamba boss huyo wa zamani wa IEBC alikuwa amelazwa katika kitengo cha wagonjwa mahututi, ambako ameripotiwa kuuga dunia leo Ijumaa 21 Feburuari 2025.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved