logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Nini kilichomuua aliyekuwa mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati, familia yafichua

Familia ya marehemu Wafula Chebukati imeeleza matukio ya kabla ya kifo chake.

image
na Samuel Mainajournalist

Yanayojiri25 February 2025 - 07:57

Muhtasari


  • Familia ya Chebukati imefichua alipambana na saratani ya ubongo hadi alipofariki kutokana na mshtuko wa moyo Ijumaa wiki iliyopita.
  • Mnamo Februari 12, 2025, Chebukati alilazwa tena hospitalini na kuwekwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).

caption

Familia ya aliyekuwa mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Wafula Chebukati, imefichua kuwa alipambana na saratani ya ubongo hadi alipofariki kutokana na mshtuko wa moyo siku ya Ijumaa wiki iliyopita.

Akizungumza wakati wa kikao na wanahabari Jumatatu, msemaji wa familia, Bw Eric Nyongesa, alieleza kuwa Chebukati aligunduliwa kuwa na saratani ya ubongo mnamo Aprili 2023, miezi michache baada ya kustaafu kutoka IEBC.

Baada ya uchunguzi huo, Chebukati alisafirishwa hadi Ujerumani ambako alifanyiwa upasuaji wa kuondoa uvimbe kwenye ubongo.

"Kwa sababu ya hatua ambayo saratani ilikuwa imefikia, madaktari walishauri afanyiwe upasuaji wa haraka. Familia yake ilizingatia chaguo mbalimbali, na hatimaye alifanyiwa upasuaji uliofanikiwa kwa kiwango kikubwa," alisema Nyongesa.

Baada ya operesheni hiyo, alikaa nchini Ujerumani kwa muda akipata nafuu hadi Julai 2023 aliporejea Kenya.

Katika kipindi hicho, hadi mwanzoni mwa 2024, Chebukati alijihusisha na shughuli mbalimbali katika mataifa ya kigeni, akishiriki midahalo kuhusu masuala ya uchaguzi.

Nyongesa alieleza kwamba mnamo Aprili 2024, uvimbe huo ulirejea, hali iliyomlazimu kurudi Ujerumani kwa upasuaji wa pili.

Baada ya kufanyiwa upasuaji huo, alibaki huko kwa muda akiendelea na matibabu hadi Agosti 2024 aliporejea Kenya kuendelea na shughuli zake za kawaida.

Hata hivyo, Desemba 2024, alipoenda hospitalini kwa uchunguzi wa kawaida, madaktari waligundua kuwa saratani hiyo ilikuwa imerejea tena. Kutokana na hali hiyo, alilazwa hospitalini hadi Januari 2025 kabla ya kuruhusiwa kurejea nyumbani.

"Alirudi nyumbani huku familia yake ikitafakari njia mbadala za matibabu, ikiwemo uwezekano wa upasuaji mwingine au mbinu zingine za kudhibiti hali hiyo," alisema Nyongesa.

Mnamo Februari 12, 2025, Chebukati alilazwa tena hospitalini na kuwekwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).

Familia ilisema kwamba mnamo tarehe 20 Februari 2025, akiwa katika matibabu, alipata mshtuko wa moyo.

"Tulipoenda hospitalini, tuliambiwa kuwa madaktari walijaribu kumuokoa lakini juhudi zao hazikufua dafu," Nyongesa alisimulia.

Aidha, familia ilikanusha uvumi uliokuwa ukienea kuhusu hali ya afya ya Chebukati, wakisisitiza kuwa hakuna wakati wowote ambapo familia iliarifiwa kuwa alikuwa amefariki kabla ya tangazo rasmi.

Nyongesa pia alithibitisha kuwa uchunguzi wa mwili wa marehemu (postmortem) utafanyika kabla ya mazishi yake, yaliyopangwa kufanyika Machi 8, 2025, katika shamba lake la Chebukati Sabata, Kitale, Kaunti ya Trans Nzoia.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved