Mwenyekiti mpya wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), Mahmoud Ali
Youssouf, ametunukiwa tuzo ya juu kabisa ya heshima na Rais wa Djibouti, Ismail
Omar Guelleh, kwa kutambua miaka yake ya kujitolea na kuhudumu kwa uadilifu
katika diplomasia.
Tuzo hiyo ilitolewa Februari 27, takriban wiki mbili baada ya Youssouf kushinda uchaguzi wa AUC mnamo Februari 15, ambapo alimshinda Raila Odinga wa Kenya na Richard Randriamandrato wa Madagascar.
Akizungumzia tuzo hiyo kupitia akaunti yake ya Twitter siku ya Ijumaa asubuhi, Youssouf alieleza furaha yake na kutoa shukrani kwa Rais Guelleh.
"Jana, Rais Guelleh alinipa tuzo ya juu kabisa ya nchi kwa miaka ya kujitolea na kazi ngumu. Sasa, ni wakati wa kufunga sura hii ya kazi yangu na kuelekea Umoja wa Afrika kuhudumia bara letu na watu wake kwa uwezo wangu wote. Nimefurahishwa sana,” Youssouf alisema.
Youssouf, mwenye umri wa miaka 59, amehudumu kama Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti tangu mwaka 2005, na ni miongoni mwa mawaziri wa muda mrefu zaidi katika nafasi hiyo barani Afrika.
Mnamo Februari 15, 2025, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa AUC baada ya kupata kura 33 kati ya 55 katika raundi ya saba ya shughuli ya upigaji kura iliofanyika Addis Ababa, Ethiopia.
Katika uchaguzi huo, waziri mkuu wa zamani wa Kenya Raila Odinga aliyekuwa na matumaini makubwa ya kushinda, aliibuka wa pili baada ya kuungwa mkono na takriban viongozi ishirini wa mataifa ya Afrika waliokuwepo.
Ushindi wa Youssouf ulionekana kama hatua kubwa kwa Djibouti katika uongozi wa masuala ya bara Afrika.
Baada ya ushindi huo, Rais Guelleh alionyesha fahari yake kwa mafanikio ya Youssouf, akisema: "Huu ni wakati wa kujivunia kwa Djibouti na Afrika. Uongozi wake utalihudumia bara kwa kujitolea na maono."
Youssouf anatarajiwa kuchukua nafasi ya Moussa Faki Mahamat wa Chad, ambaye amehudumu kama Mwenyekiti wa AUC tangu mwaka 2017.
Katika jukumu lake jipya, anakabiliwa na changamoto kubwa kama vile migogoro ya kisiasa na mapinduzi ya kijeshi katika nchi kadhaa za Afrika Magharibi, pamoja na hali tete ya usalama katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Kuchaguliwa kwake kunaleta matumaini mapya kwa Umoja wa Afrika, huku akiapa kutumia uzoefu wake wa miaka mingi katika diplomasia kuleta mabadiliko chanya na kuimarisha mshikamano kati ya mataifa ya Afrika.