Mahakama Kuu imetupilia mbali ombi la aliyekuwa Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu la kutaka aachiliwe kwa dhamana huku akisubiri kusikizwa na uamuzi wa rufaa yake.
Jaji Lucy Njuguna alisema muombaji huyo hakuishawishi mahakama kuwa rufaa yake ina nafasi kubwa ya kufanikiwa baada ya kusikilizwa.
"Ni maoni yangu kwamba waombaji hawajatimiza masharti ya dhamana. Maombi hayo yametupiliwa mbali," Jaji Njuguna alitoa uamuzi.
Jaji Njuguna pia hakukubaliana na Waititu kwamba anapaswa kuachiliwa kwa dhamana kutokana na afya yake mbaya.
"Baada ya kusikiliza nimepata kwamba waombaji hawajatimiza masharti ya dhamana. Maombi hayo yametupiliwa mbali," Jaji Njuguna alitoa uamuzi.
Waititu amekuwa gerezani tangu hakimu mkuu wa mahakama ya kupambana na ufisadi Thomas Nzyoki alipomkuta na hatia ya mgongano wa maslahi ya kushughulikia makosa ya ubadhirifu wa mali na washukiwa wengine baada ya kupokea mamilioni ya pesa kutoka kaunti ya Kiambu kupitia zabuni ya barabara ya Sh588 milioni.
Gavana huyo wa zamani wa kaunti ya Kiambu alipewa fursa ya kulipa faini ya Sh53.7 milioni au kutumikia kifungo cha miaka 12 jela.
Awali, Wakili wa Waititu Danstan Omari alikuwa amewasilisha ombi katika Mahakama Kuu akitaka akubaliwe kuachiliwa kwa dhamana ya kuridhisha akisubiri uamuzi wa rufaa aliyoiwasilisha Waititu.
Aliiomba mahakama kuruhusu dhamana aliyoweka wakati wa kesi itumike kama dhamana inayoendelea ili kupata dhamana ya kuachiliwa kwake ambayo Ilikuwa na thamani ya Sh50 milioni wakati huo.
Gavana huyo wa zamani wa Kiambu alikuwa amesema kuwa huenda akateseka iwapo ataendelea kusalia rumande kutokana na hali yake ya kiafya ya shinikizo la damu ambalo linahitaji matibabu ya dharura.
"Ninaamini kwamba rufaa ya hiyo ina nafasi ya kufanikiwa na kwamba nitabaguliwa ikiwa hukumu itatekelezwa," alisema.
Waititu alisema hakimu wa kesi hiyo Thomas Nzyoki alishindwa kuzingatia ushahidi wake na hakupima dhidi ya ule wa upande wa mashtaka katika kutoa hitimisho la haki.