logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Serikali yatangaza nafasi za kazi, Zoezi za kuajiri kufanyika Jesus Winner Ministry

Tangazo hili linajiri siku chache baada ya Askofu Edward Mwai kumwomba Rais Ruto kusaidia waumini wa kanisa lake kupata ajira.

image
na Samuel Mainajournalist

Yanayojiri04 March 2025 - 12:44

Muhtasari


  • Kwa mujibu Mutua, mpango huu ni sehemu ya juhudi za Rais William Ruto za kupanua fursa za ajira kwa vijana wa Kenya katika mataifa ya kigeni.
  • Mutua alisisitiza kuwa mpango huu unalenga kupunguza ukosefu wa ajira nchini.

Labour CS Alfred Mutua

Waziri wa Kazi, Alfred Mutua, ametangaza mpango mpya wa kuajiri Wakenya kwa kazi za ng’ambo kupitia mpango wa Kazi Majuu.

Zoezi la uajiri litafanyika katika kanisa la Jesus Winner Ministry lililopo Roysambu, Nairobi, tarehe 5 na 6 Machi 2025 kuanzia saa 2 asubuhi hadi saa 11 jioni.

Kwa mujibu wa Waziri Mutua, mpango huu ni sehemu ya juhudi za Rais William Ruto za kupanua fursa za ajira kwa vijana wa Kenya katika mataifa ya kigeni.

"Kufuatia ahadi ya Mhe. Rais Dkt. William Ruto ya kupanua fursa za ajira nje ya nchi kupitia mpango wa #KaziMajuu, kutakuwa na zoezi la uajiri katika kanisa la Jesus Winner Ministry, Roysambu, Nairobi, tarehe 5 na 6 Machi 2025," aliandika Mutua kwenye mitandao ya kijamii.

Miongoni mwa nafasi zinazotangazwa ni:

  1. Wauguzi wenye shahada kwa nafasi za kazi katika Ujerumani, Saudi Arabia, Qatar, Dubai, na Australia.
  2. Madereva wenye leseni (hasa wale waliowahi kuwa na leseni ya GCC) wanahimizwa kujiandikisha.
  3. Waendesha bodaboda za kusambaza mizigo (delivery riders) kwa nafasi zilizo Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
  4. Sekta ya hoteli: wahudumu wa hoteli, wapishi, na stewards.
  5. Sekta ya meli: mabaharia na kazi katika meli za kitalii.
  6. Sekta ya ujenzi: mafundi wa uashi, mafundi umeme, mafundi bomba, seremala, scaffolders, na vibarua wa ujenzi.
  7. Waziri Mutua alibainisha kuwa waombaji watakaofaulu watapata usaidizi kutoka kwa serikali ili kurahisisha safari yao ya ajira nje ya nchi.

"Walioteuliwa watapewa pasipoti ndani ya siku moja au mbili. Serikali pia itatoa msaada wa kifedha kwa wale wasioweza kugharamia ada za usindikaji, visa, matibabu na tiketi za ndege. Aidha, kwa baadhi ya kazi, waajiri watagharamia malazi, bima, usafiri na malipo ya saa za ziada," alisema.

Mutua alisisitiza kuwa mpango huu unalenga kupunguza ukosefu wa ajira nchini kwa kuhakikisha vijana wanapata nafasi za kazi zenye masharti mazuri na stahili bora.

Tangazo hili linajiri siku chache baada ya Askofu Edward Mwai wa Jesus Winner Ministry kumwomba Rais William Ruto kusaidia waumini wa kanisa lake kupata nafasi za ajira nje ya nchi.

"Tunao vijana hapa kanisani ambao wanatafuta ajira nje ya nchi. Wengine wamesoma lugha kama Kijerumani na Kifaransa, hivyo tunakuomba utusaidie kupata nafasi hizo," alisema Askofu Mwai.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved