Sonko alionekana kufurahisshwa na kuteuliwa kwake kwenye uongozi huo alipongeza uongozi wa muungano huo kwa kumuamini na kumpa nafasi ya kuwaongoza kitaifa.
"Leo, nimetunukiwa heshima tofauti na kuchaguliwa kwa kauli moja kama kiongozi wa Boda Boda na Tuk Tuk chama cha ushirika wa usafiri hapa Kenya.
Muungano huu unaleta pamoja Sacco na vyama vingine vyote nchi nzima chini ya mwavuli mmoja na inajivunia wanachama wanaozidi watu milioni 2.5.
Natoa shukrani zangu za dhati kwa uongozi wa muungano kwa imani waliyoiweka kwangu na uwezo wangu wa kuongoza, na nitajitolea kutetea haki zao," aliandika sonko katika ukurasa wake wa Facebook.
Gavana huyo wa zamani amesisitiza kwamba yuko tayari kipigana na wavunja sheria za muungano huo na kurejesha heshima ya wanabodaboda na waendesha tuk tuk ili kuhakikisha kuna mpangilio sahihi katika sekta hiyo.
"Kwa wahuni na wahalifu ambao wamejipenyeza katika sekta ya boda boda na kujihusisha na vitendo vya uhalifu, fahamu kuwa tutakuja kwa ajili yenu. Hatutaruhusu wahalifu wachache kuchafua jina la tasnia hii nzuri.
Chini ya uongozi wangu, ninawahakikishia watu wa Kenya njia thabiti, yenye nidhamu, na ya kitaalam ya utoaji wa huduma katika sekta hii muhimu ya usafirishaji. Nitajitolea kurejesha utulivu na usafi ndani ya sekta hii," alongeza zaidi.
Sonko awali akizungumza na wanahabari ameahidi kwamba atafanya kazi kwa karibu sana na serikali kuu na serikali za kaunti ili kuhakisha sheria zilizoko na zinazobuniwa ni nzuri na hazina athari kubwa kwa wanasekta hii ambao huitegemea ili kupata mkate wao wa kila siku.
"Moja ya masuala yanayoibuliwa na viongozi hawa ni Mswada wa Sheria ya Usafiri wa Umma (Motorcycle Regulation) wa mwaka 2023, ambao kwa sasa uko mbele ya Seneti. Wakati tunaunga mkono udhibiti wa sekta, lazima tuhakikishe kuwa sheria yoyote inayoathiri wasafiri ni ya haki, ya vitendo, na yenye manufaa kwa mamilioni ambao wanategemea tasnia hii kwa mkate wao wa kila siku. Nitashirikiana na watunga sheria, akiwemo Seneta Boni Khalwale, kuhakikisha kuwa waendesha bodaboda hawalengi haki bali wanawezeshwa kupitia mifumo sahihi inayoimarisha usalama na ustawi wao.
Zaidi ya sheria, nitashirikiana kwa karibu na serikali zote za kaunti na kitaifa kushughulikia changamoto pana zinazokabili tasnia ya bodaboda," alieleza Sonko.