
Mkutano huo utakuwa unahudhuriwa na viongozi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).
Lengo kubwa la kuwaleta pamoja viongozi hawa ni kuhusu mzozo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Kulingana na taarifa kutoka kwa SADC, Rais Ruto atakuwa mwenyekiti mwenza wa mkutano wa mtandaoni na Rais wa Zimbabwe Emmerson Dambudzo Mnangagwa.
Taarifa kutoka kwa EAC pia imethibitisha kufanyika kwa mkutano huo na kubainisha kuwa wakuu hao wa nchi watajadili ripoti iliyowasilishwa wakati wa Mkutano wa pamoja wa Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na SADC uliofanyika Machi 17, Harare nchini Zimbabwe.
“Wakuu wa nchi na Serikali za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) watafanya mkutano wao wa pili wa pamoja hii leo tarehe 24 Machi 2025 ili kushughulikia hali mbaya ya usalama katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC),"sehemu ya taarifa hiyo ilisema.
"Mkutano huo wa pamoja utaongozwa na Mheshimiwa Dkt William Samoei Ruto, Rais wa Jamhuri ya Kenya na Mwenyekiti wa EAC, na Mheshimiwa Dkt Emmerson Dambudzo Mnangagwa, Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe na Mwenyekiti wa SADC." tarifa hiyo iliendelea.
Hii itakuwa mara ya pili kwa Rais William Ruto kukutana na viongozi wa Afrika kuzungumzia mzozo wa DRC baada ya kuitisha mkutano mwingine wa dharura mwishoni mwa mwezi Januari mwaka huu.
Mapigano ya DRC yalianza mapema mwaka 2025, mapigano kati ya vikosi vya usalama vya Kongo na makundi ya wapiganaji wakiongozwa na M23 yaliongezeka kwa kasi, na kufikia kilele cha M23 kuuteka mji wa Goma.
Mnamo Februari 4, M23 ilitangaza kutositisha mapigano. Kati ya watu 900, kwa makadirio ya Umoja wa Mataifa, na watu 2,000, kwa makadirio ya serikali ya Kongo, waliuawa katika mashambulizi ya Goma.
Huku Wakongo milioni moja wakitafuta hifadhi nje ya nchi, watu milioni ishirini na moja nchini humo wanaohitaji msaada wa dharura wa matibabu, chakula, na misaada mingine, DRC inawakilisha mojawapo ya majanga makubwa na mabaya zaidi ya kibinadamu duniani.