logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Mwanawe Beatrice Elachi alifariki akisubiri kuhitimu Juni, familia yafichua mipango ya mazishi

Elvis alizaliwa Septemba 13, 1998, na atapumzishwa Machi 29, 2025

image
na Samuel Mainajournalist

Yanayojiri27 March 2025 - 09:37

Muhtasari


  • Mazishi ya mwanawe Mbunge Beatrice Elachi, yamepangwa kufanyika Jumamosi, Machi 29, 2025, katika kijiji cha Nalepo, Kaunti ya Kajiado.
  • Familia imesema kwamba Elvis, mwenye umri wa miaka 26, alikuwa kijana mwenye ndoto kubwa, na kifo chake kimeacha simanzi kubwa.

Mazishi ya mwanawe Mbunge wa Dagoretti Kaskazini, Beatrice Elachi, yamepangwa kufanyika Jumamosi, Machi 29, 2025, katika kijiji cha Nalepo, Kaunti ya Kajiado.

Katika tangazo la kifo lililochapishwa kwenye gazeti siku ya Alhamisi, familia ya Elachi ilifichua kwamba Elvis Murakana Namenya, aliyefariki Machi 25, 2025, alikuwa mwanafunzi wa Masomo ya Biashara katika Chuo Kikuu cha Africa Nazarene na alikuwa akisubiri kwa hamu kuhitimu mnamo Juni mwaka huu.

Kwa mujibu wa familia, shughuli za kumuaga rasmi zitaanza Alhamisi, Machi 28, 2025, kwa ibada ya wafu itakayofanyika katika Kanisa la Holy Trinity, Kileleshwa, kuanzia saa nne asubuhi.

Siku inayofuata, Ijumaa, Machi 29, 2025, mwili wake utaondolewa katika Lee Funeral Home saa moja asubuhi kuelekea kijijini kwao, ambapo mazishi yatafanyika kuanzia saa nne asubuhi.

Familia imesema kwamba Elvis, mwenye umri wa miaka 26, alikuwa kijana mwenye ndoto kubwa, na kifo chake kimeacha simanzi kubwa kwa familia na marafiki.

Katika ujumbe wa kumkumbuka, familia ilinukuu maneno kutoka Ayubu 1:21, yakisema:

"Nikiwa uchi nilitoka tumboni mwa mama yangu, na uchi nitarudi. Bwana alitoa, na Bwana ametwaa. Jina la Bwana lihimidiwe."

Elvis alizaliwa Septemba 13, 1998, na atapumzishwa Machi 29, 2025.

Marehemu alikaa kwa wiki moja katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) katika Hospitali ya AAR baada ya kuhusika katika ajali ya barabarani mapema wiki jana.

Inasemekana kuwa aliondoka nyumbani kuelekea Kasarani kwa shughuli zake mnamo Jumanne, Machi 18, ambapo ajali hiyo ilitokea.

Kwa bahati mbaya, alipokuwa akirejea nyumbani, gari lake lilipasuka gurudumu akiwa barabara ya Thika, na kusababisha likengeuke na kugonga uzio wa usalama.

Polisi walipofika eneo la tukio, walimkuta Elvis akiwa amepoteza fahamu na wakamkimbiza mara moja katika Hospitali ya AAR kwa matibabu ya dharura.

Hali yake ilitathminiwa na kubainika kuwa mbaya, akihitaji upasuaji wa dharura. Baada ya upasuaji, aliwekwa katika chumba cha wagonjwa mahututi kwa uangalizi zaidi. Hatimaye, alifariki dunia kutokana na mshtuko wa moyo.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved